Uchaguzi Uko Pale Pale: Majaliwa Atoa Wito kwa Wananchi, CHADEMA Yasema “No Reforms, No Election” huku Mwenyekiti Lissu Akiwa Mahabusu

 


Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 uko pale pale na maandalizi yanaendelea kama yalivyopangwa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema leo Alhamisi, Juni 26, 2025, akihitimisha Mkutano wa 19 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

Majaliwa amesema Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na hatua mbalimbali za maandalizi, huku serikali ikiahidi kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa anapata haki ya kupiga kura au kugombea bila vikwazo.

“Nitumie fursa hii kuwakumbusha wadau mbalimbali kila mmoja kwa nafasi yake, ikiwemo wananchi ambao ni wapiga kura, kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo,” amesema Majaliwa.

“Serikali itatekeleza wajibu wake wa kusimamia katiba, sheria, pamoja na taratibu zote zilizowekwa ili kila mwananchi mwenye sifa ya kuchagua na kuchaguliwa aweze kutimiza haki yake ya kikatiba bila vikwazo vya aina yoyote,” ameongeza.

Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa amani na utulivu ni tunu ya taifa inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania wakati wote wa mchakato wa uchaguzi.

“Nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha analinda na kuitunza tunu ya amani na utulivu wa nchi yetu,” amesema.

CHADEMA: Hakuna Uchaguzi Bila Mageuzi

Wakati huo huo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeendelea kushikilia msimamo wake kwamba hakuna uchaguzi huru na wa haki bila mabadiliko ya sheria, kikisema wazi kuwa: “No reforms, no election.”

Kauli hiyo imeendelea kutolewa na viongozi waandamizi wa chama hicho, wakisisitiza kuwa mazingira ya sasa ya kisiasa na kisheria hayaruhusu uchaguzi ulio wa haki na unaokubalika kwa wote.

Hata hivyo, mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, hawezi kwa sasa kushiriki moja kwa moja katika harakati hizo, baada ya kutiwa mbaroni na kuwekwa rumande kwa tuhuma za uhaini. Lissu alikamatwa mapema mwezi Mei 2025 na mpaka sasa yupo mahabusu akisubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Miongoni mwa madai yanayomkabili ni pamoja na kutoa kauli zinazodaiwa kuchochea wananchi dhidi ya serikali na kuhoji uhalali wa taasisi za uchaguzi.

Katika mahojiano ya awali kabla ya kukamatwa, Lissu alinukuliwa akisema:

“Uchaguzi wowote utakaofanyika bila marekebisho ya sheria, bila tume huru kweli, bila haki kwa vyama vyote, ni uhuni wa kisiasa. No reforms, no election.”

Msimamo huo umeungwa mkono na wanachama na mashirika ya kiraia yanayodai mageuzi ya kisiasa, huku baadhi ya wadau wa kimataifa wakifuatilia kwa karibu mwenendo wa kisiasa nchini kuelekea uchaguzi huo wa kihistoria.


0 Comments:

Post a Comment