Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwelezea Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni kiongozi mahiri aliyejidhihirisha kama nguzo ya mshikamano wa kitaifa na chachu ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini Tanzania.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Katika kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 leo tarehe 26 Juni 2025 Majaliwa amesema kuwa chini ya uongozi wake, Rais Samia ameweza kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, kukuza uchumi, na kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia. Ametaja kuwa hulka ya subira, ujasiri na uthabiti wa Rais Samia vimekuwa dira kwa viongozi wengine na matumaini kwa Watanzania.
"Ni kiongozi ambaye amekuwa alama ya matumaini kwa kizazi hiki, na mfano halisi kuwa mwanamke anaweza kuongoza kwa mafanikio hata katika nafasi ya juu ya kitaifa," amesema Majaliwa.
Aidha, amebainisha kuwa mafanikio ya uongozi wa Rais Samia yametambuliwa ndani na nje ya nchi, ambapo taasisi mbalimbali zimemkabidhi tuzo kutokana na mchango wake wa kipekee. Miongoni mwa tuzo hizo ni pamoja na Global Gates Goalkeepers, Tuzo ya Babacar Ndiaye (2022), Tuzo ya Uongozi wa Kimageuzi Afrika, na Tuzo ya Heshima ya Pyne Africa Awards (2022). Vilevile, amepokea Tuzo ya Muongoza Watalii Bora, inayoakisi mchango wake katika sekta ya utalii.
Katika ngazi ya kitaifa, Rais Samia ametunukiwa tuzo mbalimbali za heshima kutokana na juhudi zake katika maendeleo ya taifa, zikiwemo za sekta ya kilimo, elimu, tabianchi na ustawi wa jamii.
Kwa kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi na diplomasia ya kimataifa, vyuo vikuu vya ndani na nje ya Tanzania vimetunuku Rais Samia shahada za juu za Udaktari wa Heshima. Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru (India), Chuo Kikuu cha Ankara (Uturuki), na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Jamhuri ya Korea.
Majaliwa pia ametumia fursa hiyo kuwapongeza watendaji wa Serikali kwa juhudi zao za kutekeleza kwa ufanisi maono ya Rais Samia, hali iliyowezesha kupatikana kwa mafanikio makubwa katika kila sekta ya maendeleo.
Kwa ujumla, kauli ya Waziri Mkuu inaashiria imani kubwa ya Serikali na wananchi kwa uongozi wa Rais Samia, ambaye anazidi kuthibitisha kuwa Tanzania ipo katika mikono salama ya kiongozi mwenye maono, uthubutu na dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.


0 Comments:
Post a Comment