JOWUTA Yaomba Bodi ya Ithibati Kuongeza Siku za Usajili wa Wanahabari

Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kimeiomba Bodi ya Ithibati ya Wanahabari (JAB) kuongeza muda wa usajili wa wanahabari kwenye mfumo wa TAI-Habari, ili kuwawezesha waandishi wa habari kupata vitambulisho vyao vya kielektroniki (Press Card) kwa mujibu wa sheria.



Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Musa Juma, alisema licha ya pongezi kwa Bodi hiyo kwa kutekeleza wajibu wake wa kisheria, bado changamoto za kimtandao zimewafanya wanahabari wengi kushindwa kujisajili kwa wakati.

"Tunaipongeza JAB kwa kazi nzuri, lakini tunaomba muda wa usajili uongezwe angalau kwa mwezi mmoja zaidi. Kuna changamoto nyingi hasa za kimtandao ambazo zimewaathiri wanahabari kujisajili kwa wakati. Lengo letu ni kuhakikisha kila mwanahabari anafuata taratibu za kisheria na anafanya kazi kwa weledi," alisema Musa Juma.

Kwa mujibu wa JAB, kipindi cha usajili kilianza Mei 21 na kinatarajiwa kukamilika Juni 22, 2025. JOWUTA inashauri muda huo uongezwe hadi Julai 22 ili kutoa nafasi kwa wanahabari wote kukamilisha taratibu muhimu.

Katika taarifa hiyo, JOWUTA pia imewataka wanachama wake kote nchini kujisajili mapema kupitia mfumo wa TAI-Habari (https://taihabari.jab.go.tz). Kwa wanachama waliopo Dar es Salaam ambao wanakumbwa na changamoto za usajili, wametakiwa kufika katika ofisi za JOWUTA kwa msaada wa kitaalamu.

Aidha, JOWUTA imewaomba wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha wanawawezesha waandishi wao kujisajili kwa kuwawekea mazingira rafiki pamoja na kugharamia ada ya usajili ya shilingi 50,000/= kwa kila mwandishi.

Kwa mujibu wa JAB, kabla ya kujaza fomu ya maombi ya Press Card, mwandishi anatakiwa kuwa na:

  • Barua ya uthibitisho wa mwajiri au kujitegemea

  • Kitambulisho cha Taifa (NIDA)

  • Picha ndogo ya pasipoti

  • Vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa

  • Barua ya utambulisho au uthibitisho wa kazi

  • Malipo ya ada ya usajili ya Tsh 50,000 kwa njia ya kielektroniki

Viambatisho vyote vinapaswa kupakiwa katika mfumo wa PDF wakati wa kujaza fomu ya mtandaoni.

JOWUTA imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha tasnia ya habari inazingatia sheria, maadili na weledi wa kitaaluma.

0 Comments:

Post a Comment