Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Manyara, F.3544 Sajenti Ismail Rashid Katenya (49), amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi. Hukumu hiyo ilisomwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Manyara, John Kahyoza, katika Wilaya ya Babati.
Kwa mujibu wa Jaji Kahyoza, mshtakiwa alivunja masharti ya Kifungu cha 15 (1)(a), (3)(iii) cha Sheria ya Mwaka 2019 ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Sura ya 95, sambamba na ukiukaji wa Kifungu cha 18 cha Sheria Namba 5 ya Mwaka 2001, ikisomwa pamoja na Aya ya 23 ya Nyongeza ya Kwanza ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200, na Vifungu vya 57 (1) na 60 (2)(3) vya Sheria hiyo iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
"Mshtakiwa alikamatwa Januari 22, 2024 katika Kijiji cha Silaloda, Wilaya ya Mbulu, akiwa anasafirisha mirungi kilo 160.9, iliyokuwa imefungwa katika mabunda 380 ndani ya gari lake aina ya Nissan Patrol, lenye namba za usajili T 148 CTB," alisema Jaji Kahyoza.
Jaji aliongeza kuwa katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 19837 la mwaka 2024, mshtakiwa alinaswa akitokea Arusha, na upande wa mashtaka uliwasilisha vielelezo saba pamoja na mashahidi saba kuthibitisha makosa hayo.
Kwa upande wa utetezi, Wakili Fides Mwenda alimwomba Jaji amuonee huruma mshtakiwa kwa kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza, ni mtu mzima mwenye wategemezi, na maisha yake ya awali yalikuwa ya nidhamu.
"Naomba mahakama izingatie hali ya mshtakiwa na kumpunguzia adhabu, kwani hajawahi kuhusika na makosa kama haya kabla," alisema Wakili Mwenda.
Hata hivyo, mahakama haikuridhishwa na utetezi huo. Jaji Kahyoza alisisitiza kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa thabiti na wenye mashiko, na hivyo akaamua kutoa adhabu ya kifungo cha maisha.
Mahakama pia iliamuru kuwa gari lililokamatwa litakuwa mali ya Serikali endapo ndani ya siku 60 hakuna mtu atakayejitokeza kuthibitisha kuwa ni mmiliki halali wa gari hilo.
Kesi hiyo imeibua hisia mbalimbali miongoni mwa wananchi wa mkoa wa Manyara, huku wengi wakilaani vitendo vya askari kutumia nyadhifa zao vibaya na kushiriki katika biashara haramu ya dawa za kulevya.

0 Comments:
Post a Comment