Zaidi ya watu 100 wamethibitishwa kufariki dunia kufuatia mafuriko makubwa yaliyolikumba kijiji cha Kasaba, kilichopo kandokando ya Ziwa Tanganyika katika eneo la Fizi, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa Samy Kalodji, msimamizi wa eneo la Fizi katika jimbo la Kivu Kusini, ripoti kutoka eneo hilo zinaonesha kuwa “zaidi ya vifo 100” vimeripotiwa hadi kufikia Jumamosi.
Mafuriko hayo yanatokea wakati taifa hilo la Afrika ya Kati linakabiliwa na hali ya taharuki inayochangiwa na kuongezeka kwa mashambulizi ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika eneo la mashariki mwa nchi, mashambulizi ambayo yameua maelfu tangu mwanzo wa mwaka huu.
Didier Luganywa, msemaji wa serikali ya mkoa wa Kivu Kusini, alisema mafuriko hayo yalitokea “kati ya Alhamisi usiku na Ijumaa wakati wa mvua kubwa na upepo mkali, hali iliyosababisha mto Kasaba kuvunja kingo zake.”
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali ya mkoa, hadi sasa vifo 62 vimeweza kuthibitishwa rasmi, huku watu wengine 30 wakiwa wamejeruhiwa.
Eneo la Kasaba, lililoathirika vibaya, lina changamoto za mawasiliano kwani halijafikiwa na mtandao wa simu za mkononi na linaweza kufikika kwa njia ya maji kupitia Ziwa Tanganyika pekee — hali inayokwaza juhudi za haraka za uokoaji na misaada ya kibinadamu.

0 Comments:
Post a Comment