CHARLES HILARY AFARIKI DUNIA: MZEE WA CHARANGA KUZIKWA ZANZIBAR

  


Mtangazaji mashuhuri na gwiji wa habari, Charles Hilary, ameaga dunia alfajiri ya leo Jumapili, akiwa hospitalini Mloganzila, Dar es Salaam. Taarifa rasmi ya Ikulu ya Rais wa Zanzibar imethibitisha kifo hicho, ikisema marehemu alikuwa akihudumu kama Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Hilary “alikimbizwa hospitalini baada ya kuugua ghafla akiwa nyumbani kwake” kabla ya kufariki dunia.

Charles Hilary, ambaye amejizolea umaarufu mkubwa Afrika Mashariki, alianza kazi yake ya utangazaji katika Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) mwanzoni mwa miaka ya 1980. Aliibuka kuwa miongoni mwa sauti za dhahabu kwenye matangazo mubashara ya mpira wa miguu.

Mwaka 1994, alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa kituo cha Radio One Stereo jijini Dar es Salaam na kupata umaarufu zaidi kupitia kipindi cha muziki wa charanga, akipachikwa jina la “Mzee wa Charanga.”

Alihamia Idhaa ya Kiswahili ya DW nchini Ujerumani mwaka 2003 na baadaye kujiunga na BBC Idhaa ya Kiswahili mwaka 2006, ambako alihudumu kwa miaka tisa. Akiwa BBC, Hilary alijulikana kwa umahiri wake kwenye vipindi vya habari na Ulimwengu wa Soka, kilichokuwa kikitangaza Ligi Kuu ya England kila wikendi.

Mwaka 2012, alihusishwa na uzinduzi wa televisheni ya Dira TV, na mwaka 2015 aliondoka BBC na kurejea nyumbani Tanzania, ambako alijiunga na Azam TV kabla ya kuteuliwa kuwa msemaji wa Ikulu ya Zanzibar mwaka 2021.

Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alitoa salamu za rambirambi akisema: “Tumempoteza mchapakazi, mzalendo na kiongozi aliyejituma kwa weledi mkubwa katika utumishi wa umma.”

Familia ya marehemu pia imethibitisha kifo hicho na kueleza: “Alikumbwa na maradhi ya ghafla nyumbani kwake, na alihamishiwa hospitalini mara moja, lakini hatukufanikiwa kumuokoa.”

Kwa sasa, mipango ya mazishi inaendelea kuratibiwa na familia kwa kushirikiana na serikali ya Zanzibar.


0 Comments:

Post a Comment