![]() |
| Wajumbe wa Urusi (kulia) na Ukraine wakifanya mazungumzo nchini Uturuki. |
WAZIRI wa Ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov, amesema kuwa Ukraine na Urusi zimefikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa wa vita 1,000 kutoka kila upande, ikiwa ni moja ya matokeo ya mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni kati ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na wanahabari wa Ukraine, Umerov alisema: "Tumejadili suala la kusitisha mapigano na suala la kubadilishana wafungwa. Matokeo yake ni kubadilishana watu 1,000 kwa 1,000. Hayo ni matokeo ya mkutano wetu."
Ingawa tarehe rasmi ya utekelezaji wa makubaliano hayo haijawekwa wazi, Waziri Umerov alithibitisha kuwa tayari imepangwa.
Aidha, alifichua kuwa katika mazungumzo hayo, pia ulijadiliwa uwezekano wa kufanyika kwa mkutano wa ana kwa ana kati ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Alisema taarifa zaidi kuhusu duru mpya ya mazungumzo zitatangazwa hivi karibuni.
Makubaliano haya yanakuja wakati vita kati ya mataifa hayo mawili yanaendelea kuleta madhara kwa raia na kuongeza shinikizo la kimataifa la kutafuta suluhu ya amani ya kudumu.


0 Comments:
Post a Comment