Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameonyesha kutoridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne, akiutaja kuwa na kiwango kikubwa cha uzembe unaosababisha usumbufu kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Mwenge hadi Tegeta, na kutoka Mwenge hadi Ubungo, Waziri Ulega alieleza kushangazwa na namna wasimamizi na mshauri elekezi wanavyoshindwa kuchukua hatua dhidi ya mkandarasi anayeonekana kupuuzia taratibu za utekelezaji wa kazi.
“Mimi nimepita kukagua. Kazi ambazo nimeaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni za barabara na madaraja. Rais hapendi na hafurahishwi na msongamano mkubwa hapa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini. Hisia hizo hajawahi kuzificha,” alisema Ulega.
Katika eneo la Palm Beach, Upanga, Waziri huyo alikuta shimo kubwa limechimbwa na mkandarasi wakati bado hajakamilisha kazi katika maeneo ya awali ya mradi kutoka Morocco, Mwenge hadi Kaunda. Kitendo hicho kilimuudhi na kumfanya kuhoji sababu ya kuanza kazi mpya bila kumaliza sehemu za mwanzo.
“Nini kimemfanya awe na haraka ya kuja kutifua huku wakati kule hajakamilisha? Hii ndiyo hoja yangu na ugomvi wangu hapa,” alisema.
Amebaini kuwa tatizo kubwa lipo kwa wasimamizi wa mradi pamoja na mshauri elekezi, ambao kwa mujibu wake, wamekosa uadilifu na kuzembea katika majukumu yao.
“Hii ni barabara ya umma, si mali ya mkandarasi. Mkandarasi hawezi kuvamia na kuchimba kiholela. Hapa shida si mkandarasi peke yake, ni wasimamizi na mshauri elekezi,” alisisitiza.
Kutokana na kile alichokiona, Waziri Ulega ameagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kumpatia taarifa kamili ya wasimamizi wote wa mradi pamoja na mshauri elekezi ili kufanyika uchunguzi wa kina.
“Haiwezekani ikawa tu ni uzembe wa kawaida, inaweza kuwa kuna jambo linafichwa,” alisema.
Amesema yuko tayari kuchukua hatua kali dhidi ya mkandarasi ikiwa ataonekana kushindwa kwenda sambamba na kasi ya serikali.
“Yawezekana wale wanaotakiwa kunishauri kwa uaminifu, wamehamia upande wa mkandarasi. Kazi yao ni kunisaidia, si kuficha uzembe,” alieleza.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Rajabu Iddi, aliwaomba radhi wananchi kwa usumbufu wanaoupata kutokana na ujenzi huo, na kusisitiza kuwa wanajitahidi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
“Tunaendelea kusimamia mradi kwa juhudi kubwa kuhakikisha unakamilika kwa wakati,” alisema Rajabu.
Aliongeza kuwa wameweka mikakati ya kupunguza usumbufu kwa wananchi ikiwemo matangazo ya mara kwa mara na njia mbadala za kupita.
Mradi wa BRT Awamu ya Nne, sehemu ya kwanza, unahusisha jumla ya vituo 18 vya mabasi ya mwendokasi na unatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari jijini Dar es Salaam mara utakapokamilika.


0 Comments:
Post a Comment