TLS Yaomba Serikali Magari kwa Ajili ya Kutoa Msaada wa Kisheria Pembezoni, Yasema "Kwenda Mahakamani Si Vita"

 



Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeiomba serikali kuwapatia magari saba kwa ajili ya kanda zake saba ili kuimarisha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.



Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa chama hicho, Rais wa TLS Boniface Mwabukusi alisema kuwa kuna changamoto kubwa ya miundombinu inayokwamisha mawakili kufika maeneo ya mbali ambako wananchi wanahitaji msaada wa kisheria.

"Tulikuwa tunaomba serikali ione umuhimu wa kuipatia TLS magari saba kwa ajili ya hizo kanda ili kutekeleza wajibu ilio nao wa kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, legal aid kwa watu walio pembezoni," alisema Mwabukusi.

Aliongeza kuwa chama hicho kinatambua wajibu wake wa kuimarisha utawala wa sheria kwa uaminifu, upendo na utii kwa mamlaka, na kusisitiza kuwa hawana maslahi binafsi bali wanalinda maslahi ya Taifa.

"Tunapotekeleza wajibu wetu watu watuvumilie kwa sababu hatuna maslahi binafsi ila ulinzi wa Taifa letu kwa uaminifu," alisema.



Katika hotuba yake, Mwabukusi alielezea kusikitishwa kwake na baadhi ya watu wanaozuia wananchi kwenda mahakamani, akieleza kuwa ni haki ya msingi kwa kila mtu kusikilizwa na kuona mifumo ya haki inavyofanya kazi.

"Juzi nimeona watu wanaenda mahakamani limekuwa zoezi la kivita, nimeona cinema za akina Amita Bachan... watu wanaeuka kuzuia watu wasiende mahakamani. Kwenda mahakamani ni haki, watu waende wakasikie, wakaone haki ikitendeka," alisema.

Aidha, TLS kimeishauri serikali kuanzisha chombo maalum cha kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi hususani yanayohusu haki za binadamu na utawala bora, kikisema kuwa chombo hicho kinapaswa kuwa na mamlaka kamili na uwezo wa kutoa maelekezo yenye uzito kama amri za mahakama.



Akizungumzia masuala ya Utawala Bora na Katiba Mwabukusi amesema, "Kumekithiri vitendo vya Utekaji na kupotea kwa watu TLS inatoa Rai kwa kuundwa kwa chombo huru kinachoweza kusimamia Law enforcement Agency, Uwezi kupeleka police kesi inayowahusu waichunguze wenyewe,".


Mkutano huo wa mwaka wa TLS umeongozwa na kauli mbiu isemayo "Uchaguzi na utawala wa sheria: wito wa uangalizi wa kisheria na uwajibikaji katika mfumo wa uchaguzi wa Tanzania."

Akielezea kauli mbiu hiyo, Mwabukusi alisema: "Kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa misingi ya utawala wa kisheria inazingatiwa katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi kuanzia maandalizi, upigaji kura hadi utoaji wa matokeo."



Kwa upande wake, Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Boniface Simbachawene, alipongeza TLS kwa mchango wake katika kuimarisha utawala bora na demokrasia nchini.

"TLS ni muhimu katika kutoa miongozo ya kisheria na kuhamasisha demokrasia," alisema Simbachawene.



Aliongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na TLS katika juhudi za kuboresha mifumo ya kisheria na utawala bora, huku akisisitiza kuwa mabadiliko ya kikatiba na kisiasa yanapaswa kuzingatia maoni ya wananchi.




0 Comments:

Post a Comment