“HAKI ITANGULIE KABLA YA MAENDELEO” ASEMA PAUL MAKONDA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kiasi cha shilingi bilioni 42.34 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha walioguswa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Fidia hiyo inalenga kumaliza migogoro ya ardhi na kuwezesha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama vile ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, maeneo ya jeshi, na shughuli za uchimbaji madini.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Moshono jijini Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita imejikita katika kulinda haki za wananchi kabla ya kusukuma mbele ajenda ya maendeleo.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inalenga kuhakikisha kuwa haki inatendeka kabla ya maendeleo yoyote kufanyika. Hatuwezi kuendelea huku kuna watu wanapoteza makazi yao bila fidia stahiki,” alisema Makonda.
Kwa mujibu wa Makonda, malipo ya fidia yameshafanyika katika maeneo kadhaa kama ifuatavyo:
-
Eneo la Jeshi la Losirwa, Jiji la Arusha – shilingi bilioni 2.27 (tayari imelipwa).
-
Eneo la Oloresho, kwa maandalizi ya mashindano ya AFCON – shilingi bilioni 7.27.
-
Barabara ya Mianzini – Ngaramtoni – shilingi bilioni 3.49 (tayari imelipwa).
-
Barabara ya Mirongoine – Olmot – shilingi milioni 591.64 (tayari imelipwa).
-
Eneo la Jeshi, Duluti, Wilaya ya Arumeru – shilingi bilioni 7.9 (tayari imelipwa).
-
Uwanja wa ndege wa Manyara, Wilaya ya Karatu – shilingi bilioni 5.9.
-
Eneo la Engaruka, Wilaya ya Monduli (uchimbaji wa madini ya magadi soda) – shilingi bilioni 14.9.
Makonda alieleza kuwa fedha hizo ni ushahidi wa dhamira ya serikali katika kuhakikisha kwamba maendeleo hayajengwi juu ya mateso ya wananchi, bali kwa usawa na haki kwa wote.
“Sitaki kusikia mwananchi anaondolewa kwenye ardhi yake bila kulipwa haki yake. Hii siyo serikali ya kufanya mambo kwa mabavu. Huu ni utawala wa sheria, haki na maendeleo ya wote,” alisisitiza.
Aidha, Makonda aliwataka viongozi wote wa halmashauri, wilaya na taasisi za serikali ndani ya mkoa huo, kuzingatia misingi ya haki wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Kiongozi yeyote atakayehusika kuwaondoa wananchi bila kuwapa fidia, ajue anakwenda kinyume na maelekezo ya serikali ya awamu ya sita. Hatuwezi kukubali kuona wananchi wetu wanapoteza mali zao kwa sababu ya uzembe wa viongozi,” alisema.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo walipokea taarifa hiyo kwa furaha, wakisema ni hatua kubwa inayodhihirisha utawala wa haki na usawa unaosisitizwa na serikali ya sasa.
Miongoni mwa miradi inayotajwa kufanikishwa kutokana na fidia hizi ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, upanuzi wa viwanja vya ndege, pamoja na uwekezaji katika sekta ya madini ambao unatajwa kuongeza ajira na pato la taifa.
“Tunashukuru sana kwa hatua hii. Serikali imetutendea haki na sasa tuko tayari kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” alisema mkazi mmoja wa eneo la Losirwa.
Hii ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa dhamira ya serikali ya kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika safari ya maendeleo ya kitaifa.













0 Comments:
Post a Comment