RAMAPHOSA KUKUTANA NA TRUMP KATIKA ZIARA YA KIKAZI MAREKANI, LENGO NI KUFUFUA UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA

 


Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi nchini Marekani wiki ijayo ambapo atakutana na Rais wa Marekani, Donald Trump, mnamo Mei 21 katika Ikulu ya Marekani, Washington DC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa Afrika Kusini siku ya Jumatano, "Rais Ramaphosa atakutana na Rais Donald Trump katika Ikulu ya Marekani huko Washington DC kujadili masuala ya maslahi ya pande mbili, kikanda na kimataifa."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Ziara ya rais nchini Marekani inatoa fursa ya uwepo wa uhusiano mpya wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili."

MIGOGORO YA KIDIPLOMASIA NA KUSITISHWA KWA MISAADA

Uhusiano kati ya Afrika Kusini na Marekani umedorora tangu Donald Trump arejee madarakani mwezi Januari. Serikali ya Trump imechukua msimamo mkali dhidi ya Afrika Kusini, hatua iliyopelekea kusitishwa kwa misaada yote ya kifedha kutoka Marekani.

Trump amenukuliwa akieleza kuwa uamuzi huo unatokana na "kutoridhishwa na sera ya Afrika Kusini ya mageuzi ya ardhi" pamoja na "kesi dhidi ya mshirika wetu Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki."

Sera ya mageuzi ya ardhi ya Afrika Kusini inalenga kurekebisha usawa wa umiliki wa ardhi uliorithiwa kutoka enzi za ubaguzi wa rangi, ambapo ardhi kubwa bado inamilikiwa na wachache, hasa wazungu. Hata hivyo, Marekani imeeleza wasiwasi wake kuhusu uhalali wa utaratibu wa mageuzi hayo na athari zake kwa wawekezaji wa kimataifa.

Mgogoro huo ulizidi kuchacha wiki hii baada ya utawala wa Trump kuwapokea Wazungu 49 kutoka Afrika Kusini na kuwapa hadhi ya ukimbizi, akiwachukulia kuwa ni “waathirika wa ubaguzi wa rangi.” Hatua hiyo imezua mjadala mkali ndani na nje ya Afrika Kusini, huku ikionekana kama ishara ya kutokuwa na imani na sera za serikali ya Ramaphosa.

ZIARA YENYE UZITO MKUBWA KIDIPLOMASIA

Ziara ya Ramaphosa inachukuliwa kama juhudi ya kutuliza hali ya sintofahamu na kurejesha uhusiano wa karibu na Marekani, ambao kwa miaka mingi umekuwa wa kimkakati katika nyanja za biashara, ulinzi, afya na uwekezaji.

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaitazama ziara hii kama fursa muhimu kwa Afrika Kusini kuwasilisha msimamo wake, kueleza mantiki ya sera zake za ndani, na kujenga upya mawasiliano ya moja kwa moja na Washington, huku ikiangazia pia masuala ya usalama wa kikanda, biashara huria barani Afrika, na ushirikiano wa kimataifa.

Taarifa zaidi kuhusu matokeo ya mkutano huu mkubwa zinatarajiwa baada ya Mei 21.

0 Comments:

Post a Comment