Wananchi wa Manyire Waanza Rasmi Ujenzi wa Sekondari Yao, Wamshukuru Dkt. Lukumayi na Rais Samia

 


WANANCHI wa Kijiji cha Manyire, Kata ya Mlangarini mkoani Arusha, wameanza rasmi ujenzi wa shule yao ya sekondari. Hatua hii inaleta ukombozi mkubwa wa kielimu na kumaliza changamoto ya muda mrefu ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.


Utekelezaji wa mradi huo umeanza kushika kasi kufuatia Serikali kutoa fedha za awamu ya kwanza. Tayari mradi umekabidhiwa rasmi, ambapo wananchi kwa kushirikiana na mkandarasi wapo kazini kuchimba msingi wa majengo ya shule hiyo.

Diwani wa Kata ya Mlangarini, Emanuel Mrema, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi huo unaogusa maisha ya wananchi.

"Ujenzi wa shule hii ni faraja kubwa kwa wananchi wa Manyire ambao kwa miaka mingi walikosa shule ya sekondari karibu. Watoto wetu walilazimika kutembea hadi kilomita 24 kila siku kufuata masomo, jambo lililoathiri mahudhurio na maendeleo yao kitaaluma," alisema Mrema.

Mrema alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumayi, kwa juhudi zake za kupigania mradi huo bungeni. Pia aliishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Arusha chini ya Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Selemani Msumwi, kwa ushirikiano uliowezesha mradi kuanza.


Alibainisha kuwa vijana wa eneo hilo wamejitokeza kwa wingi kushiriki hatua za awali za ujenzi. Diwani huyo aliwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana na kulinda miradi ya maendeleo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

"Watoto wetu hawapaswi kurithi migogoro au visasi. Wanapaswa kurithi miradi ya maendeleo itakayoboresha maisha yao na kuwasaidia kufikia ndoto zao," alihitimisha Mrema.

0 Comments:

Post a Comment