Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, leo asubuhi amefanya ziara ya ukaguzi katika eneo la ujenzi wa madaraja mawili ya King’ori yanayojengwa kwenye barabara kuu ya Arusha–Moshi. Madaraja hayo ni sehemu muhimu ya miundombinu inayounganisha mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, na ni mkombozi mkubwa kwa usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma.
Akiwa katika eneo la ujenzi, Makonda ameonesha kuridhishwa na kasi na viwango vya utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kuwa serikali inalenga kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto za usafiri zilizokuwa zikiathiri maisha ya wananchi, hasa wakati wa mvua.
“Serikali ina wajibu wa kulinda maisha ya wananchi wake, ndiyo maana tumetafuta suluhu ya kudumu kwa kujenga daraja imara badala ya makalvati yaliyokuwa yakisababisha madhara. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo katika kuhakikisha usalama wa barabara hii muhimu,” amesema Makonda.
Ameongeza kuwa ujenzi huu ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na maendeleo ya miundombinu, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia kwa vitendo agenda ya uboreshaji wa barabara nchini.
“Natoa pongezi kwa Rais wetu kwa maono makubwa na msisitizo katika kuhakikisha miundombinu ya barabara inaboreshwa na kuwa salama – iwe ni kipindi cha mvua au kiangazi,” amesema.
Makonda pia ameipongeza Wizara ya Ujenzi pamoja na taasisi zote zinazoshiriki utekelezaji wa mradi huo kwa kazi nzuri wanayoifanya, huku akisisitiza kuwa maendeleo haya hayapaswi kuchukuliwa kirahisi.
Aidha, amewakumbusha watumiaji wa barabara hiyo kufuata sheria za usalama barabarani ili kuhakikisha miundombinu hii inadumu kwa muda mrefu, hasa kutokana na umuhimu wake kwa sekta ya utalii na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa kaskazini.
Mradi wa ujenzi wa madaraja hayo unatekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa gharama ya shilingi bilioni 4.6, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Julai 2, 2025.








0 Comments:
Post a Comment