Wanafunzi wa Kidato cha Nne 2024 Wapewa Fursa ya Kubadili Machaguo ya Tahasusi na Kozi

 



Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amesema kwamba wanafunzi waliomaliza Kidato cha Nne mwaka 2024 wanayo nafasi ya kubadili machaguo ya tahasusi (Combination) na kozi mbalimbali kulingana na ufaulu wao.



Waziri Mchengerwa alitoa kauli hiyo leo, Aprili 2, 2025, Jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu fursa hii ya kubadili machaguo ya tahasusi na kozi. 

Alisema kuwa rasmi sasa wahitimu wa Kidato cha Nne wa mwaka 2024 wanaweza kubadilisha machaguo ya tahasusi za Kidato cha Tano, vyuo vya kati, na elimu ya ufundi kupitia mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Tano na vyuo hivyo.

“Zoezi la kubadilisha tahasusi na vyuo lilianza rasmi Machi 31, 2025, na litakamilika Aprili 30, 2025. 


Hivyo, wanafunzi, wazazi, na walezi wanakumbushwa kushauriana kikamilifu, ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalamu na kitaaluma, kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au kozi,” alisema Mchengerwa.

Aidha, Waziri Mchengerwa alisisitiza kuwa TAMISEMI inatoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya Sekondari wa mwaka 2024 kubadili machaguo yao ili kuwawezesha kusoma tahasusi au kozi itakayowaandaa kupata utaalamu stahiki kwa maisha yao ya baadaye.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa mchakato huu, wahitimu wote wanahimizwa kufanya marekebisho ya machaguo yao ya tahasusi na kozi kulingana na ufaulu wao kwa kuingia kwenye Mfumo wa Uchaguzi wa Wanafunzi (Student Selection MIS), unaopatikana kupitia kiunganishi cha selform.tamisemi.go.tz,” aliongeza Mchengerwa.

Waziri Mchengerwa alisisitiza kuwa huduma ya kubadilisha tahasusi ni bure, na iwapo wanafunzi watakumbana na changamoto, wanapaswa kuwasiliana na Dawati la Huduma kwa Mteja kupitia barua pepe: huduma@tamisemi.go.tz au kupiga simu kwa namba +255 262 160 210 na +255 735 160 210.

Itakumbukwa kuwa serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya tahasusi na kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi (Selform). Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).

0 Comments:

Post a Comment