Fisi Wavamia Nyumba Waua Kondoo 21, Wengine Tisa Hawajulikani Walipo

 


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, kundi la fisi limevamia nyumbani kwa Mageni Maduhu, mtaa wa Mahina, kata ya Somanda, Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoani Simiyu na kuua kondoo wake 21, huku wengine tisa wakiwa hawajulikani walipo. 



Tukio hili lilitokea jana, Aprili Mosi, 2025, majira ya saa nne usiku, na kushangaza wengi katika eneo hilo.

Mageni Maduhu akisimulia tukio hilo alisema, "Nilianza kusikia mlio wa fisi mmoja majira hayo ya usiku, nikatoka nje na kuanza kumkimbiza. 


Lakini baada ya kumkimbiza fisi huyo, nilikutana na kundi jingine la fisi ndipo nilipoamua kurudi nyumbani. Nilipofika kwenye zizi la kondoo, niliwakuta kondoo wangu wakiwa wamekufa na damu nyingi."

Maduhu alieleza kuwa, "Kwenye zizi kulikuwemo kondoo 30, ambapo 21 walishambuliwa na kufa. Kondoo wengine 9 hawapo hadi sasa, na baadhi ya kondoo walikuwa na mimba na wameuawa. Fisi walikuwa wengi sana."

Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahina, Mangu Mangolyo, alizungumzia tukio hilo na kusema, "Tukio hili linashangaza kwani halijawahi kusikika au kuonekana fisi wakishambulia au kula kondoo wengi kiasi hiki. Nilifika kwenye tukio na kukuta kondoo wote wakiwa wamekufa."

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, ambaye alifika kwenye eneo la tukio, alisema, "Mpaka sasa bado tunaendelea na uchunguzi kubaini kama ni kweli fisi ndiyo wametenda tukio hili au la. Vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na mamlaka ya wanyamapori, vinaendelea na uchunguzi."

Aliongeza kusema, "Tunatoa pole kwa familia iliyokubwa na tukio hili, na tunatangaza kuanza rasmi kwa msako wa fisi katika maeneo yote yenye vichaka kwenye Halmashauri ya Mji wa Bariadi. Tumeanza kupata taarifa za uwepo wa fisi katika maeneo haya."

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alitoa tahadhari kwa wananchi, akisema, "Tunaomba watu wote wanaodaiwa kufuga wanyama hawa kuacha mara moja, kwani msako huu utahusisha pia watu wote wanaomiliki fisi. Tutachukua hatua kali kwa wanaofuga fisi."

Tukio hili limeongeza hofu miongoni mwa wakazi wa Mji wa Bariadi, na operesheni ya kupambana na wanyama hao inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo.

0 Comments:

Post a Comment