Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, alikutana jana mjini Kinshasa na Massad Boulos, mshauri wa rais wa Marekani Donald Trump.
Mazungumzo yao yalijikita katika uwezekano wa kufikia makubaliano kuhusu uchimbaji madini ya Kongo, ingawa hawakufafanua iwapo kutakuwa na ushirikiano wa kiusalama kati ya mataifa hayo mawili.
Massad Boulos, ambaye ni Mmarekani aliyezaliwa Lebanon na ameolewa na Tiffany Trump, binti wa Rais Donald Trump, ni mshauri mkuu wa Afrika kwa Trump na pia mshauri mkuu katika masuala ya Mashariki ya Kati. Boulos alizuru DRC kwa lengo la kujadili masuala ya uwekezaji wa madini na mchango wa Marekani katika juhudi za amani mashariki mwa Kongo, eneo lilio na migogoro ya muda mrefu.
Marekani ipo katika mazungumzo ya kuwekeza mabilioni ya dola katika sekta ya madini ya Kongo, hasa kutokana na utajiri wa madini ya cobalt, lithiamu, uranium, na madini mengine ambayo ni muhimu kwa magari ya umeme na teknolojia ya simu. Hivi karibuni, Marekani imeonyesha nia ya kuongeza uwepo wake katika sekta hii ili kuimarisha ushirikiano na DRC, ambapo sehemu kubwa ya uchimbaji madini inatawaliwa na makampuni ya China.
Akizungumza baada ya mkutano na Rais Tshisekedi, Boulos alisema, “Washington imechunguza pendekezo la madini ya DRC kwa ajili ya usalama na kukubaliana juu ya njia ya kusonga mbele.” Hata hivyo, aliongeza kuwa maelezo ya mpango huo bado hayajafichuliwa kwa umma.
"Umesikia kuhusu mkataba wa madini. Tumepitia pendekezo la Congo, na rais na mimi tumekubaliana juu ya hatua zitakazochukuliwa," alisema Boulos katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, kama ilivyoripotiwa na Reuters.
Boulos alionyesha kuwa makampuni ya sekta binafsi ya Marekani yatakuwa muhimu katika ushirikiano wowote utakaofanyika, akisisitiza kuwa, “Uwe na uhakika, makampuni ya Marekani yanafanya kazi kwa uwazi na yatachochea uchumi wa ndani. Huu ni uwekezaji wa mabilioni ya dola."
DRC, ambayo ni mojawapo ya mataifa yenye utajiri mkubwa wa madini duniani, ina akiba kubwa ya madini muhimu kwa teknolojia ya kisasa.
Huu ni mfano mwingine wa jinsi mataifa makubwa yanavyoshindania rasilimali za kimsingi zinazohitajika katika uchumi wa dunia wa sasa.

0 Comments:
Post a Comment