Mahakama ya Kikatiba ya Korea Kusini imetangaza uamuzi wa kihistoria kwa kuunga mkono kuondolewa madarakani kwa Rais Yoon Suk Yeol, baada ya kupiga kura kwa kauli moja kumtaka ashtakiwe kwa matumizi mabaya ya madaraka.
Uamuzi huu unahitimisha mchakato wa kumvua Rais Yoon madarakani, huku wananchi wa Korea Kusini sasa wakiwa na muda wa siku 60 kufanya uchaguzi wa haraka kujaza nafasi yake.
Jaji wa Mahakama ya Kikatiba, Moon Hyung-bae, alitoa hukumu ya mwisho akieleza kuwa hatua ya Rais Yoon ya kutekeleza agizo la kijeshi ilikuwa ni ukiukwaji wa haki za kimsingi za kisiasa za raia.
Aliongeza kuwa hatua hiyo pia ilikiuka kanuni za utawala wa sheria na demokrasia, na kwamba matumizi ya nguvu yalikuwa kinyume na sheria.
"Hakutekeleza wajibu wake na alikwenda kinyume na raia ambao alipaswa kuwalinda," alisema Jaji Moon.
Rais Yoon alikumbwa na lawama baada ya kutuma wanajeshi bungeni ili kuzuia shughuli za bunge, hali ambayo ilizua mivutano kati ya serikali na upinzani.
Mahakama iligundua kuwa hakuna hali ya dharura ya kitaifa ambayo ingeweza kuhalalisha hatua hiyo, na badala yake ilieleza kuwa suala hilo lingeweza kutatuliwa kwa njia nyingine isiyohusisha matumizi ya jeshi.
Jaji Moon aliongezea, "Hakukuwa na hali ya dharura ya kitaifa. Ilikuwa hali ambayo ingeweza kutatuliwa kwa njia nyingine zaidi ya kutumwa kwa jeshi."
Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Han Duck-soo, ambaye pia ni kaimu rais wa nchi hiyo, alieleza kuwa atahakikisha hakuna mapungufu katika usalama wa taifa na diplomasia, na kwamba utulivu wa umma utadumishwa.
Katika hotuba ya televisheni, Han Duck-soo alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama na utulivu katika kipindi hiki cha mpito.
"Kama kaimu rais, nitaweka msimamo thabiti wa kiusalama ili kuhakikisha hakuna mapungufu katika usalama wa taifa na diplomasia.
Aidha, nitafanya kila jitihada kuhakikisha hakuna ucheleweshaji wa kushughulikia masuala muhimu kama vile vita vya biashara, na nitahakikisha utulivu wa umma ili wananchi wasiishi kwa wasiwasi," alisema Han.
Rais Yoon alikumbwa na mgogoro wa kisiasa mwaka jana, baada ya kutangaza sheria ya kijeshi kuhusiana na mgogoro wa bajeti kati yake na bunge.
Hatua hii ilimpelekea kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na bunge, na hatimaye, kumvua madaraka.
Uamuzi huu wa Mahakama ya Kikatiba unaashiria mabadiliko makubwa katika siasa za Korea Kusini, na huenda ukawa na athari kubwa kwa usalama wa taifa na utawala wa nchi.
Wakati Rais Yoon anajiandaa kuondoka madarakani, sasa inabaki kuona jinsi uchaguzi wa haraka utaathiri mustakabali wa taifa hili lenye nguvu kubwa kiuchumi na kisiasa katika Asia.
0 Comments:
Post a Comment