Tasnia ya Urembo Yampoteza Hashim Lundenga "Uncle Hashim"





Tasnia ya urembo nchini  imepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Hashim Lundenga, maarufu kwa jina la “Uncle Hashim”, aliyefariki dunia leo jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Lundenga alikuwa mwanzilishi na Mkurugenzi wa kampuni ya Lino International Agency, ambayo ilisimamia mashindano ya Miss Tanzania kwa zaidi ya miaka 23. Kupitia uongozi wake, mashindano haya yalipata umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi, na kuwapa warembo wa Kitanzania fursa ya kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa kama Miss World.

Mwaka 2018, baada ya kulitumikia shindano hilo kwa miongo miwili, Lundenga alikabidhi rasmi usukani kwa Basila Mwanukuzi, Miss Tanzania wa mwaka 1998. Hatua hiyo ilikuja baada ya changamoto na migogoro ya mara kwa mara iliyokuwa ikiathiri mwenendo wa mashindano hayo.

Mbali na mchango wake mkubwa kwenye tasnia ya urembo, Lundenga pia alikuwa mchango muhimu katika sekta ya michezo, hasa kupitia klabu ya Yanga SC, ambako alihudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi.

Alitambulika kwa uwezo wake wa kugundua na kukuza vipaji, akiwatoa warembo waliokuja kuwa watu mashuhuri kama Jackline Ntuyabaliwe (K-Lyn), Millen Magese, Nancy Sumari, Faraja Kota, na Wema Sepetu – wote ambao waliiwakilisha Tanzania vyema kitaifa na kimataifa.

Kwa zaidi ya miongo miwili, Hashim Lundenga alikuwa nguzo kuu ya mashindano ya Miss Tanzania tangu yalipoanzishwa mwaka 1994 hadi alipojiondoa rasmi kutokana na changamoto za kiuendeshaji. Kifo chake kimeacha pengo kubwa na huzuni katika sekta ya urembo na burudani nchini.

0 Comments:

Post a Comment