Wananchi Walalamikia Kusambaa kwa Chuma Chakavu Barabarani, Diwani Msofe Atia Neno

 


Wananchi wa kata ya Daraja Mbili jijini Arusha wamelalamikia hali ya kusambaa kwa chuma chakavu kwenye barabara ya Matilda Matokeo, ambapo wafanyabiashara wa chuma chakavu, ikiwemo machuma mabati, wanaendesha shughuli zao. 



Hali hii inasababisha magari na waenda kwa miguu kutumia eneo dogo lililobaki, hali inayochangia msongamano mkubwa na kero kwa watumiaji wa barabara.



https://youtu.be/lkcjG27IZlU?si=t5dj1sOCdGQSbIq8


Wananchi hao, ambao wameomba majina yao yasichapishwe kwa kuhofia usalama wao, wamesema kuwa wameshafikisha malalamiko yao kwa viongozi wa serikali lakini hawajaona hatua yoyote inayochukuliwa. 



"Ulipita pale kwa gari ni tabu tupu, kwanza inabidi kusubiriana wapite wa upande mmoja wakimaliza ndiyo wa upande mwingine upite, lakini wakati mwingine ukipita unakuta tairi imepata pancha kwa sababu pale kuna mabati, chuma na misumari," alisema mmoja wa wananchi hao.




Mmoja wa wafanyabiashara wa chuma chakavu, Nickson Shirima, alieleza kuwa machuma hayo yanatolewa kutoka kwenye godown na kupelekwa kiwandani. Alisisitiza kuwa wao hawaruhusu kuweka vitu nje ya eneo hilo. 


"Hivi vitu hapa vimetolewa godown vinapelekwa kiwandani. Hapa huwa hatuweki vitu nje," alisema Shirima. 


Aliongeza kuwa malalamiko ya watu kuumia kwa pancha na kushindwa kupishana barabarani yanaweza kuwa yanatokana na magari makubwa ya kubeba maji taka yanayopita eneo hilo.




Diwani wa Daraja Mbili, Prosper Msofe (CCM), alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kusema kuwa suala hilo lipo chini ya serikali. 


"Ilitakiwa tangu Desemba 20, 2024 wawe wameondoa vitu vyote pale lakini nimesikia bado hawajaondoa. 


Na kwa kuwa mmekuja kiniuliza, naomba niwahakikishie kwamba ndani ya wiki hii tutahakikisha Mtendaji anachukua hatua ya kuwaondoa pale," alisema Diwani Msofe.




Msofe aliongeza kuwa wafanyabiashara hao walikuwa waliahidi kutafuta maeneo mengine ya kufanyia biashara lakini hadi sasa hawajatekeleza ahadi hiyo. "Tutachukua hatua kuhakikisha wale mabwana wanapisha. 


Na wale wengine wote wanaoendesha shughuli zao kwenye maeneo ya barabara wapishe ili wasigeuke kero kwa watumiaji wengine," alisisitiza.


Kwa upande wake, Mtendaji wa kata ya Daraja Mbili, Anzamen Sawe, alisema kwamba wafanyabiashara wa chuma chakavu walishatolewa notisi na kuandikiwa barua, lakini hawakutekeleza maagizo hayo. "Nilishawaandikia barua waondoke lakini hawajatekeleza, ngoja tuone tutafanya nini kwa sababu walikodisha lile godown kwa ajili ya kuingiza vitu ndani lakini cha kushangaza bado anaweka vitu nje," alisema Sawe.


Hata hivyo, juhudi za kumpata mfanyabiashara mwingine aitwaye Selemba, ambaye anahusika na shughuli za chuma chakavu, hazikuzaa matunda baada ya kutokuwepo eneo hilo. Simu yake haikupokelewa, na wafanyakazi wake walieleza kuwa boss wao alikuwa ametoka.


Wananchi wamesisitiza kuwa wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira ni wa kila mmoja, na wanaomba viongozi kuchukua hatua za haraka ili kumaliza kero hii inayoathiri usalama na usafiri wa watu.

0 Comments:

Post a Comment