Shirika la Anga la Kenya (KSA) limethibitisha uwepo wa taarifa hizo na kuwataka wananchi wa Kenya kuwa makini na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama iwapo watashuhudia chombo au chuma chochote kikubwa kikidondoka kutoka angani katika maeneo yao. Aidha, wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara ya kimwili.
Ingawa taarifa hiyo haijabainisha kwa uhakika ni nchi au eneo gani ambalo kifaa hicho kitaangukia, KSA imeeleza kuwa mabaki hayo yanatarajiwa kupita katika anga ya Afrika Mashariki, ikiwemo maeneo kadhaa ya Kenya. Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na mamlaka za Tanzania kuhusu tukio hilo.
Kwa mujibu wa KSA, mabaki ya roketi hiyo, yenye uzito ambao haujafahamika, yanatarajiwa kuingia tena katika anga ya dunia Jumamosi tarehe 19 Aprili 2025 majira ya saa 5:15 usiku (11:15pm). Hata hivyo, muda huo unaweza kubadilika kwa mapema au kuchelewa kwa takriban saa 15 na dakika 46, hivyo kuifanya tarehe ya kuingia kuwa kati ya Jumamosi saa 1:29 asubuhi (7:29am) hadi Jumapili saa 9:01 mchana (3:01pm), tarehe 20 Aprili 2025.
KSA imeeleza kuwa licha ya kutotarajiwa kuanguka moja kwa moja ndani ya mipaka ya Kenya, ukubwa wa kifaa hicho unaweza kuleta madhara kwa maisha ya watu na mali endapo kitaangukia maeneo yenye makazi. Tukio kama hili lilishuhudiwa Januari 2025, ambapo chuma kinachodhaniwa kuwa mabaki ya roketi kilianguka katika kijiji cha Makuku, kaunti ya Makueni, na kuleta taharuki kwa wakazi. Mabaki hayo yalikuwa na kipenyo cha takriban mita 2.5 na uzito wa takriban kilo 500.
Kwa kawaida, vifaa kama hivi hutengenezwa kwa namna ya kuteketea angani vinapoingia tena kwenye anga ya dunia au kuanguka katika maeneo yasiyo na makazi ya watu.
"Iwapo utaona kifaa au chuma chochote kikubwa kimeanguka kutoka angani, tafadhali toa taarifa kwa kituo cha polisi kilicho karibu nawe, na usijaribu kukigusa kwa sababu kinaweza kuwa hatari kwa afya yako au kusababisha majeraha," imesema taarifa ya KSA.
Chanzo: BBC

0 Comments:
Post a Comment