Biteko Avutiwa na Utekelezaji wa Miradi ya Hospitali ya Wilaya Arumeru na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ameonyesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Arumeru, hususan mradi wa kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Arumeru na ujenzi wa jengo la utawala la Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, (TCDI).



Akizungumza Aprili 25, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tengeru, Dkt. Biteko alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 100 katika miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.



"Arusha DC imepokea zaidi ya shilingi bilioni 49.6, na Arumeru imepokea zaidi ya shilingi bilioni 51 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hili ni jambo kubwa, wananchi wana kila sababu ya kumshukuru Rais kwa jitihada hizi," alisema Dkt. Biteko.





Alitaja mafanikio yaliyopatikana kupitia uwekezaji huo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme kwa vijiji vingi, ujenzi wa shule, maabara, vituo vya afya, hospitali, miradi ya barabara, pamoja na miradi ya kilimo. 



Aidha, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika ambazo zimefanikiwa kuzalisha umeme kwa asilimia 100.



Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Biteko alieleza kuwa Serikali bado inafanya kazi ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya maji, barabara na miundombinu mingine.

"Serikali ni sikivu. Tutahakikisha barabara zinazohitajika zinajengwa, daraja na huduma za maji zinapatikana. Tutaendelea kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi," aliongeza.

Aliwahimiza wananchi kudumisha amani, mshikamano na uzalendo kwa Taifa. 



“Tusijaribu kuichezea amani. Ni msingi wa maendeleo yote. Rais Samia ameapa kuilinda kwa gharama yoyote, na sisi wote tuna jukumu hilo,” alisema Dkt. Biteko.


Akihimiza ushiriki wa wananchi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, alisema: “Kauli mbiu yetu mwaka huu ni ‘Muungano wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa; Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025’. Tuchague viongozi watakaolinda na kuendeleza miradi ya maendeleo.”



Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alisema kuwa mkoa umeweka kipaumbele katika uboreshaji wa miundombinu, hasa sekta ya barabara. 


Alisema fedha zaidi ya shilingi milioni 270 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Resingita na milioni 105 kwa barabara ya Longido–Meloe.

"Tunapongeza wananchi kwa kuelewa kuwa maendeleo ni mchakato, na madiwani pamoja na wabunge wamekubaliana kuwa kipaumbele chetu cha mwaka 2025/26 ni barabara," alisema Makonda.



Akizungumzia miradi ya nishati, alisema: "Wananchi sasa wanaunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kupitia mradi wa REA, na vijiji na vitongoji vyote vitakuwa na umeme ifikapo mwishoni mwa mwaka huu"


Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru. 


Mradi huo, wenye thamani ya shilingi bilioni 5.664, unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 17, 2025.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha TCDI, Dkt. Bakari George, hadi sasa ujenzi huo umeshagharimu shilingi bilioni 2.7. 


Jengo hilo litakuwa na ghorofa tatu na sakafu nne, likiwa na jumla ya ofisi 44 pamoja na kumbi tano zitakazoweza kuchukua watu 545 kwa wakati mmoja.


Dkt. Biteko yupo katika ziara ya siku tano mkoani Arusha, ambapo tayari ametembelea wilaya za Monduli, Longido na Arumeru, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

0 Comments:

Post a Comment