Biteko Aipongeza AUWSA kwa Kufanikisha Upatikanaji wa Maji kwa Asilimia 99.2



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) kwa hatua kubwa ya mafanikio katika utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira, baada ya kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa asilimia 99.2 — zaidi ya lengo la Serikali la kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.



Pongezi hizo zimetolewa Aprili 26, 2025, wakati Dkt. Biteko alipotembelea kituo cha kusambaza maji cha AUWSA kilichopo Chekereni, wilayani Arumeru mkoani Arusha.

“Niwapongeze kwamba kiwango cha maji mnachozalisha ni kikubwa kuliko mahitaji, manake ni kwamba upatikanaji wa maji umefika asilimia 99. Hii ni hatua kubwa sana,” alisema Biteko.



Aidha, alihimiza umuhimu wa kuwa na vyanzo mbadala vya nishati, akieleza kuwa tatizo la umeme linaweza kuathiri moja kwa moja upatikanaji wa maji.



“Ikitokea umeme umekatika, backup yenu ni nini?” alihoji Biteko, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba, alieleza kuwa mamlaka hiyo ipo katika hatua za awali za kuandaa mazingira kwa wawekezaji binafsi kuwekeza katika mfumo wa nishati ya jua (sola).

“Lengo letu ni kuhakikisha kila kituo cha pampu kinakuwa na chanzo mbadala cha umeme ili kuondoa utegemezi wa gridi pekee,” alisema Rujomba.

Katika taarifa yake kwa Naibu Waziri Mkuu, Rujomba alieleza kuwa mafanikio hayo yamepatikana kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa thamani ya Shilingi Bilioni 520, unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

“Kupitia mradi huu, tumeweza kujenga matanki 11 ya kuhifadhi maji, ambapo kwa sasa tuna uwezo wa kuhifadhi lita milioni 40 kwa siku. Tenki kubwa lina ujazo wa lita milioni 10. Hata maji yakikatika, tunaweza kuendelea kutoa huduma kwa saa nane bila changamoto yoyote,” alisema Rujomba.

Katika upande wa majitaka, AUWSA imepanua mtandao wa ukusanyaji kutoka asilimia 8.03 mwaka 2020/21 hadi asilimia 39.5 mwaka 2024/25. Pia imenunua magari matano ya kunyonya majitaka yenye uwezo wa kubeba kati ya lita 5,000 na 10,000.

“Majitaka yanayokusanywa kutoka kwa wateja zaidi ya 10,930 yanatibiwa katika mabwawa ya kisasa yaliyopo Kata ya Terati, yenye uwezo wa kutibu lita milioni 22 kwa siku. Awali, mabwawa hayo yalikuwa na uwezo wa lita milioni 3.5 pekee,” alisema.

Rujomba alieleza kuwa muda wa upatikanaji wa huduma ya maji umeongezeka kutoka saa 16 mwaka 2020 hadi saa 22 mwaka 2025. Idadi ya wateja waliounganishwa na huduma za maji pia imeongezeka kutoka 71,183 mwaka 2021 hadi 134,000 kwa sasa.

Pamoja na mafanikio hayo, Biteko alieleza wasiwasi wake kuhusu kiwango kikubwa cha upotevu wa maji, akisema:

“Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA, asilimia 49 ya maji yanapotea kabla hayajafika kwa wateja. Kwa kuwa uko kwenye eneo lenye wateja wengi, hakikisha unatafuta suluhisho la kudhibiti upotevu huu,” alisema.

Aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu bili zisizoendana na matumizi.



“Mkiona wananchi wanalalamika kuwa bili ni kubwa kuliko matumizi, hilo ni jambo linalowahusu moja kwa moja. Hakikisheni mnalidhibiti,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Rujomba, maeneo yanayohudumiwa na AUWSA ni pamoja na Jiji la Arusha, Monduli, Ngaramtoni, USA River, Mererani, na Longido – likijumuisha kata za Namanga na Kimokou – kwa jumla ya wakazi 1,076,523 kulingana na sensa ya mwaka 2022.

Mradi mkubwa uliofanyika unahusisha upatikanaji wa maji safi, uondoaji wa majitaka, na uimarishaji wa uwezo wa taasisi. 



AUWSA imejenga mtambo wa kutibu maji safi katika chanzo cha Midawe unaoweza kutibu lita milioni 10 kwa siku, ofisi kuu katika eneo la Safari City pamoja na ofisi nne za kanda.



“Kwa sasa tunaweza kusema AUWSA ndiyo mamlaka ya kwanza nchini yenye mabwawa bora na yenye uwezo mkubwa wa kutibu maji taka. Pia tumefanikisha kuchimba visima 56, viwili kati ya hivyo vikitoa maji kwa nguvu ya asili bila mashine – jambo linalosaidia wananchi kuendelea na kilimo hata visima hivyo vikiwa havifanyi kazi,” alieleza Rujomba.



Akitamatisha ziara yake, Dkt. Biteko alisema:

“Fedha zilizowekwa hapa ni nyingi mno, zaidi ya bilioni 500. Ni lazima fedha hizi zitafsiri maisha bora ya watu. Maisha hayawezi kuwa bora kama hakuna maji. Maji hayana mbadala.”


0 Comments:

Post a Comment