TCRA: Vyama Vyote Vipewe Nafasi Kwenye Vyombo vya Habari Wakati wa Uchaguzi

 



Meneja wa Kitengo cha Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, amesisitiza kuwa vyombo vya habari nchini vinapaswa kuzingatia maadili ya uandishi na utangazaji, hasa wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu. 


Amewataka waandishi wa habari kuhakikisha wanaripoti habari kwa usawa, haki na bila upendeleo, ili kutoa taarifa sahihi zitakazowawezesha wananchi kufanya maamuzi bora.


"Vyama vyote vya siasa vinapaswa kupatiwa nafasi sawa katika kuripotiwa, bila upendeleo. Hii itasaidia kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zinazowawezesha kufanya maamuzi ya busara," alisema Mhandisi Kisaka akiwa kwenye Mkutano wa Misa Tanzania na Wadau (MISA-TAN – Wadau Summit 2025) uliofanyika jijini Dodoma.

Mhandisi Kisaka aliongeza kuwa vyombo vya habari vina jukumu muhimu la kuripoti kwa usahihi na kuzingatia maadili, ili kuepuka upotoshaji wa taarifa. Alihimiza waandishi wa habari kutenda haki kwa kuripoti kile kilichotokea kama kilivyokuwa, na kuepuka kuongeza "chumvi" au kubuni matukio.

“Ni muhimu waandishi wa habari kutotoa habari ambazo hazina ukweli. Tunapaswa kuripoti kwa usahihi na kwa umakini, hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi," alisema.

Vilevile, Mhandisi Kisaka alisisitiza kuwa waandishi wanapaswa kuzingatia kuripoti sera na ahadi za vyama vya siasa, badala ya kuzingatia matukio pekee, ili kuwaelimisha wananchi kuhusu mipango ya vyama na jinsi wanavyokusudia kutatua changamoto zinazowakumba.

“Hii itasaidia kuelimisha umma kuhusu mipango ya vyama vya siasa na jinsi wanavyokusudia kutatua changamoto zinazowakumba wananchi,” alifafanua.

Kwa kumalizia, Mhandisi Kisaka alisisitiza kuwa ni jukumu la vyombo vya habari kuhakikisha wanaripoti kwa haki, usawa, na uadilifu, ili kulinda demokrasia ya nchi na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa zinazowafaidi.

0 Comments:

Post a Comment