Arusha Kuunganishwa na Mtandao wa SGR, Bunge Laombwa Kuunga Mkono Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo




Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Christian Makonda, ameishukuru serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia kuanza kwa uvunaji wa madini ya magadisoda katika eneo la Engaruka Monduli, hatua inayotarajiwa kuvutia uwekezaji mkubwa wa takribani Dola bilioni 1.5 za Kimarekani. 

Serikali tayari imetoa kiasi cha bilioni 14 kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaothirika na utekelezaji wa mradi huo. 

Makonda aliahidi kuwa atasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hii ili kuhakikisha inakuwa na tija kwa wananchi na serikali.


Makonda aliyasema hayo leo, Ijumaa Machi 14, 2025, alipokutana na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Jijini Arusha, ambapo aliwasilisha ajenda mbalimbali zinazohusiana na maendeleo ya mkoa wa Arusha. 


Miongoni mwa ajenda hizo ni pamoja na mpango wa serikali wa kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka mkoani Tanga hadi mkoani Arusha, na kuunganishwa na mpango mwingine wa ujenzi wa bandari kavu mkoani Arusha, itakayounganishwa na Bandari ya Tanga.



Akizungumzia kuhusu umuhimu wa bandari ya Tanga, Makonda alisema kuwa bandari hiyo ni ya pili kwa kupokea shehena nyingi zaidi za mizigo nchini, ikitokana na uwekezaji wa takribani Bilioni 500 zilizowekezwa na serikali. 


Hali hii imepelekea barabara za Arusha kuwa na msururu mrefu wa malori, ambapo idadi ya malori imeongezeka kutoka 60 hadi 600 kwa siku, yakielekea nchi za nje. 


Hivyo, alisisitiza kuwa kujengwa kwa reli ya kisasa kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo na kupunguza msongamano wa malori barabarani.


Makonda alieleza kuwa mradi huu wa SGR ni muhimu kwa maendeleo ya mkoa wa Arusha na taifa kwa ujumla, kwani utarahisisha biashara na usafiri kati ya nchi za Afrika Mashariki na nchi nyingine. 

Aliongeza kuwa reli hiyo itasaidia katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kuleta manufaa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha.



Vilevile, Makonda aliwaomba wajumbe wa kamati hiyo ya bunge kuunga mkono juhudi za serikali kwa kuhakikisha kuwa mpango huu wa ujenzi wa reli ya kisasa unatekelezwa kwa haraka. 

Alisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati kama hii utaleta maendeleo ya kudumu kwa mkoa wa Arusha na nchi nzima.




Katika kumalizia, Makonda alitoa wito kwa bunge na serikali kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inayopitishwa inatekelezwa kwa ufanisi na kwa haraka, ili wananchi wa mkoa wa Arusha na maeneo mengine ya nchi waweze kufaidika na matunda ya juhudi za serikali.

0 Comments:

Post a Comment