RAIS SAMIA: MRADI WA MAJI SAME-MWANGA-KOROGWE NI UKOMBOZI KWA WANANCHI

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe ni hatua kubwa ya ukombozi kwa wananchi wa wilaya za Same, Mwanga na Korogwe.



Akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, mara baada ya kuzindua rasmi mradi huo, Rais Samia alisema mradi huo umeongeza uwezo wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Same-Mwanga kufikisha maji safi na salama kwa wananchi kutoka watu 50,615 hadi 300,000 katika vijiji 38.



"Mradi huu umekuwa mkombozi kwa wananchi wa wilaya hizi kwa sababu umeimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa idadi kubwa ya watu. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi hawapati shida ya maji," alisema Rais Samia.



Katika ziara hiyo ya kikazi ya siku moja, Rais Samia alitembelea Bwawa la Nyumba ya Mungu na kuweka jiwe la msingi la mradi huo, akisisitiza kuwa serikali haitakubali kushindwa katika kuwaletea wananchi maendeleo.

"Siwezi kuamini katika kushindwa. Nawaomba watumishi wa umma kuwa na moyo wa kupambana ili kuhakikisha miradi kama hii inakamilika na kuwanufaisha wananchi," alisisitiza.



Aidha, aliiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha awamu ya pili ya mradi huo inatekelezwa kwa ukamilifu ili kuimarisha upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Korogwe.



"Natamani kuona awamu ya pili ya mradi huu inatekelezwa haraka ili huduma ya maji iwe bora zaidi kwa wananchi wa Korogwe," alisema Rais Samia.

Pia, alisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa sekta ya maji, akiwataka kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu katika maeneo yenye miundombinu ya maji.

"Ni wajibu wenu kuwahudumia wananchi kwa weledi na kwa wakati. Pia, hakikisheni vyanzo vya maji vinalindwa ili serikali itimize ahadi yake kwa wananchi," aliongeza.

Mradi wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe ni miongoni mwa miradi mikubwa inayotekelezwa na serikali kwa lengo la kuboresha huduma ya maji safi na salama nchini.

0 Comments:

Post a Comment