Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amewasihi wananchi waliojiajiri kujiunga na kuchangia mfuko huo ili kujihakikishia usalama wa baadaye dhidi ya majanga kama uzee, maradhi na ulemavu.
Akizungumza tarehe 7 Machi, 2025, katika Soko la Kilombero jijini Arusha, Mshomba alikutana na wananchi waliojiajiri wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini, machinga, bodaboda, wasanii, wasusi, wafanyabiashara wa masoko, pamoja na mamalishe na babalishe.
"Kwa muda mrefu, wananchi waliojiajiri hawakuwa na fursa ya kunufaika na mafao ya hifadhi ya jamii, lakini sasa serikali imefungua milango kwao kujiunga na NSSF ili waweze kupata mafao yote yanayotolewa, yakiwemo mafao ya matibabu," alisema Mshomba.
Alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri yanayowezesha wananchi waliojiajiri kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya sasa na ya baadaye.
Mshomba aliwahimiza wananchi waliojiajiri kujiunga kwa wingi na kuchangia NSSF, akisema kuwa kwa kufanya hivyo, wanajihakikishia maisha bora baada ya kustaafu kazi au kukumbwa na changamoto za kiafya. "Wanaojiunga na kuchangia NSSF ndio ‘Mastaa wa Mchezo’ wa baadaye kwa sababu watanufaika na mafao mbalimbali na huduma za hifadhi ya jamii," alisisitiza.
Alieleza kuwa serikali imeweka utaratibu rahisi wa usajili na uchangiaji ili kuwawezesha wananchi kujiunga kwa urahisi. "Sasa, wananchi waliojiajiri wanaweza kujiunga NSSF kwa kupiga 15200# na kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi au msimu," alisema Mshomba.
Mkurugenzi huyo aliwashukuru wale waliokwisha jiunga na mpango huo na kueleza kuwa lengo la NSSF ni kuhakikisha wananchi wote waliojiajiri wanapata elimu ya hifadhi ya jamii, wanajiunga na kujiwekea akiba ili kupunguza umasikini nchini.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Soko la Kilombero, Rajabu Hassan, aliishukuru serikali kupitia NSSF kwa kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri. "Hii ni fursa nzuri kwa watu kujenga maisha bora kwa kuweka akiba zao kwa utaratibu rasmi," alisema.
Naye, Mkurugenzi wa Uwekezaji, Mipango na Miradi wa NSSF, Gabriel Silayo, aliwahamasisha wananchi waliojiajiri kutumia fursa ya kampeni ya "NSSF Staa wa Mchezo" kwa kujiunga na mfuko huo ili wanufaike na mafao yanayotolewa.
Kampeni hii ni sehemu ya juhudi za serikali za kuongeza ujumuishaji wa kifedha na ulinzi wa kijamii kwa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uhakika wa maisha yake ya sasa na ya baadaye.





0 Comments:
Post a Comment