INEC Yaongeza Siku Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Dar

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC) imetangaza kuongeza siku mbili zaidi za zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo zoezi hilo litamalizika rasmi tarehe 25 Machi 2025





Hatua hiyo ilitangazwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, leo tarehe 23 Machi 2025, kufuatia mwitikio mkubwa wa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki kwa wingi katika zoezi la uboreshaji ambalo lilianza tarehe 17 Machi 2025 na lilitarajiwa kumalizika leo, Machi 23 mwaka huu.

"Hivyo basi, napenda kuwatangazia wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa, Tume imeongeza siku mbili za uboreshaji wa Daftari kwa tarehe 24 na 25 Machi, 2025 na zoezi litakamilika tarehe 25 Machi 2025 saa 12:00 jioni," alisema Jaji Mwambegele.

Aidha, Jaji Mwambegele alifafanua kuwa baada ya siku hizo mbili, Tume haitaongeza muda zaidi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

"Wakati zoezi linaendelea, Tume imeongeza mashine za BVR pamoja na watumishi ili kutoa huduma bora na kwa haraka," alisema Jaji Mwambegele. "Kutokana na mwitikio mkubwa, Tume ilichukua hatua za kuongeza mashine za BVR kits pamoja na watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi, na hatua hii imewezesha zoezi kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote," aliongeza.

Jaji Mwambegele aliongeza kuwa mwitikio wa wananchi umewezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa misongamano kwenye baadhi ya maeneo na kuboresha kasi ya kuwahudumia watu. Alitoa pongezi kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa mara ya kwanza, kuboresha taarifa zao, na kupata kadi mpya kwa wale waliopoteza au kuharibu kadi zao.

Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi kuwa zoezi hili halihusishi kubadilisha kadi za wapiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020.

"Napenda kuwakumbusha kuwa zoezi hili halihusishi ubadilishaji wa kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 kwa kuwa kadi hizo ni halali na zitaendelea kutumika kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani," alisema Jaji Mwambegele.

"Kwa hiyo, wananchi wote ambao kadi zao hazijaharibika au kupotea, wala hawajahama kutoka kata au halmashauri, hawahusiki na zoezi hili," aliongeza.

Pia, Jaji Mwambegele aliwaonya wananchi kuhusu kosa la kujiandikisha zaidi ya mara moja. Alisema kuwa kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kisheria, na mtu yeyote atakayekutwa na kosa hilo anaweza kufungwa jela, kutozwa faini, au vyote kwa pamoja.

"Mtu yeyote akithibitika amejiandikisha zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani," alieleza.

Mwisho, Jaji Mwambegele alitoa wito kwa wadau wote wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na wananchi, kutoa ushirikiano kwa Tume na kuhakikisha kuwa wanaokwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao vituoni ni wale tu ambao wanastahili kufanya hivyo.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mikoa 30, na mzunguko huu wa 13 unahusisha Mkoa wa Dar es Salaam pekee.

0 Comments:

Post a Comment