Biteko; Tunapojitahidi Kuhifadhi Vyanzo vya Maji, Tunazuia Migogoro ya Maji na Mazingira

 


"Tusipotunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira tutajikuta katika mtanziko mkubwa (water stress)," amesema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, akiongeza kuwa kukosekana kwa rasilimali maji kwa baadhi ya watu kunaweza kuwa chanzo cha migogoro na machafuko katika jamii husika.




Dkt. Biteko ameyasema haya jijini Dar es Salaam leo Machi 19, 2025, wakati wa uzinduzi wa taarifa ya utendaji wa Mamlaka za Maji kwa mwaka 2023/24. Alisema kwamba upatikanaji wa huduma za maji ni haki ya msingi kwa kila raia, na hivyo ni muhimu kulinda vyanzo vya maji ili kuwezesha upatikanaji wake.



"Jamii ina wajibu wa kuhakikisha usafi wa mazingira, kupanda miti, na kuhifadhi misitu ili kuendelea kupata na kutumia rasilimali maji," alisisitiza Dkt. Biteko.

Ili kukabiliana na changamoto hii, na kumwezesha kila Mtanzania kupata huduma za maji na usafi wa mazingira, Dkt. Biteko aliielekeza Mamlaka za Maji kupunguza kiwango cha upotevu wa maji, jambo ambalo limekuwa chanzo cha hasara kubwa. 


Aliweka wazi kuwa hasara ya shilingi bilioni 114.12 ilitokana na upotevu wa maji kwa mwaka huu pekee.

Hadi sasa, asilimia 84 ya maeneo ya mijini na asilimia 79.6 ya maeneo ya vijijini zimeunganishwa na huduma za maji, huku kukiwa na ongezeko la asilimia 7 kutoka kipindi cha mwaka uliotangulia.



Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisisitiza kuwa kumekuwa na ongezeko la ubora wa viwango vya maji na udhibiti wa upotevu wa maji. 


"Upotevu wa maji unaleta hasara kubwa hasa unapothamanishwa kifedha," alisema Aweso, akipongeza pia EWURA kwa kazi nzuri na kutoa taarifa inayoonesha uhalisia wa mambo. 

Alisema kwamba mamlaka zinazofanya vizuri zinapata tuzo, na kwamba hii ni motisha ya ushindani wa kimaendeleo.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Profesa Mark Mwandosya, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya maji, akisema bajeti ya sekta hiyo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 206 mwaka 2010/11 hadi shilingi bilioni 558 mwaka 2024/25.

Profesa Mwandosya alisema kwamba uwekezaji katika sekta ya maji unaleta faida kubwa, na akatoa mfano kuwa uwekezaji wa dola 1 katika sekta ya maji unaweza kuleta faida ya dola 7 katika uchumi wa taifa.



Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andelile, alikiri mafanikio yaliyopatikana, lakini pia alitaja changamoto zinazotokana na utegemezi wa Mamlaka za Maji kwa Serikali. 

Alisema kuwa uchakavu wa miundombinu ya maji ni changamoto nyingine inayosababisha upotevu wa maji na hasara kwa Serikali.

Dkt. Andelile pia alieleza kwamba baadhi ya Mamlaka za Maji zimefanya vizuri katika udhibiti wa upotevu wa maji. 



Mamlaka zilizofanya vizuri ni Maganzo (4%), Nzega (6%), Kashuwasa (11%), Biharamulo (12%), na Mwanuzi (13%). 


Hata hivyo, alionyesha kuwa baadhi ya mamlaka zimekuwa zikishindwa kudhibiti upotevu wa maji kwa kiwango kikubwa, ikiwa ni pamoja na Rombo (70%), Handeni (69%), Mugango/Kyabakari (68%), Ifakara (56%), na Kilindoni (55%).

Dkt. Biteko, akiwa mgeni rasmi, alitoa tuzo na vyeti kwa Mamlaka za Maji zilizofanya vizuri katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

0 Comments:

Post a Comment