Wakuu wa Hifadhi za Taifa Wampongeza Kamishna Kuji kwa Juhudi Zake za Kuboresha Uhifadhi na Utalii



Wakuu wa Hifadhi za Taifa nchini Tanzania wamempongeza Kamishna wa Uhifadhi, Musa Juma Kuji, kwa juhudi zake za kujitolea kwa kiasi kikubwa na kuwatembelea maafisa na askari wa Uhifadhi katika maeneo yao ya kazi. 



Kamishna Kuji amekuwa akifanya vikao na maafisa hao ili kuwasikiliza, kuwapa ushauri, na kuwatia moyo, jambo ambalo limeleta tija kwa watumishi na kuongeza morali ya kazi.


“Afande Kamishna tunakushukuru na kukupongeza sana kwa uamuzi wako wa kufanya ziara za kutembelea hifadhi na kukutana na maafisa na askari katika vituo vyao kwani jambo hilo limesaidia sana kutatua changamoto zilizopo. 


Hivyo watumishi wamekuwa wakipata faraja na kuongeza morali ya utendaji kazi, hongera sana afande,” alisema Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Charles Ngendo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Rumanyika-Karagwe.



Kamishna Kuji alifanya kikao kazi na Wakuu wa Hifadhi za Taifa zote 21 mjini Dodoma tarehe 18 Machi 2025, kwa lengo la kufanya tathmini ya hali ya uhifadhi na utalii nchini. 


Katika kikao hicho, aliwasisitiza Wakuu wa Hifadhi kuongeza jitihada katika utendaji kazi ili kuboresha ukuaji wa utalii na kuongeza mapato kwa Taifa.


“Tuendelee kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa tunabuni mazao mapya ya utalii ambayo yatakuwa na matokeo ya kuongeza mapato ndani ya shirika na serikali kwa ujumla. 



Pia, nakubaliana na ushauri wenu wa kuongeza nguvu ya kuyafikia masoko ambayo yanaongoza kuleta watalii wengi wanaotembelea Hifadhi za Taifa,” alisema Kamishna Kuji.


Wakuu wa Hifadhi walipata fursa ya kujadili masuala muhimu ya kuboresha utendaji kazi na kuinua kiwango cha utoaji huduma kwa watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa Tanzania. 


Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linasimamia jumla ya hifadhi 21, na kila hifadhi ina Mkuu wa hifadhi ambaye ni Afisa wa cheo cha juu cha maamuzi ya mwisho kwa ngazi ya hifadhi husika, akiwa kiungo muhimu katika usimamizi na uratibu wa shughuli za uhifadhi na utalii nchini.

0 Comments:

Post a Comment