Washington – Rais wa Marekani Donald Trump amesisitiza tena kuwa nchi yake itachukua udhibiti wa Ukanda wa Gaza, hatua inayozua mjadala mkubwa kimataifa.
Akizungumza katika Ikulu ya White House Jumanne, Trump alikutana na Mfalme Abdullah wa Jordan kwa mara ya kwanza tangu atangaze pendekezo la kuchukua eneo hilo na kuwahamisha Wapalestina milioni mbili katika nchi nyingine za Kiarabu, ikiwemo Jordan.
Mapema wiki hii, Trump alidai anaweza kuzuia msaada wa Marekani kwa Jordan na Misri isipokuwa wakubali kuwachukua Wapalestina kutoka Gaza.
Hata hivyo, Jordan, ambayo tayari ni nyumbani kwa mamilioni ya Wapalestina, imekataa mpango huo.
Baada ya mkutano wao, Mfalme Abdullah alisema: "Msimamo thabiti wa Jordan [ni] dhidi ya kuhama kwa Wapalestina."
Pia unaweza kusoma zaidi https://habaritanzaniagracemacha.blogspot.com/2025/02/rais-wa-palestina-akataa-vikali.html
Licha ya msimamo huo, Trump alisisitiza kuwa bado anashikilia pendekezo lake. Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval huku Mfalme Abdullah akiwa ameketi karibu naye, Trump alisema: "Tutaichukua. Tutaishikilia. Tutaienzi."
Trump pia alidai kuwa ikiwa Marekani italichukua Gaza, eneo hilo litakuwa na maendeleo makubwa. "Ajira nyingi zitaundwa katika eneo lote," alisema.
Pendekezo la Trump limeibua shutuma kali kutoka kwa mataifa ya Kiarabu na jamii ya kimataifa, huku wengi wakiona kama jaribio la kulazimisha mabadiliko ya kisiasa na kidemografia katika Mashariki ya Kati.

0 Comments:
Post a Comment