Dkt. Ntuli Kapologwe, Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara ya Afya Tanzania, ameibuka mshindi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC) baada ya kuwashinda wagombea wengine sita waliokuwa wakiwania nafasi hiyo.
Dkt. Kapologwe anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Prof. Yoswa Dambisya wa Uganda, ambaye amehudumu kwa mihula miwili ndani ya miaka 10. Kwa mujibu wa vigezo vya Jumuiya hiyo, ataongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza baada ya zoezi la uchaguzi Februari 12, 2025, Waziri wa Afya wa Tanzania, Jenista Mhagama, alisema: “Nafasi hiyo ilipotangazwa kwa mara ya kwanza, jumla ya waombaji 47 waliwasilisha wasifu wao, na kati yao, saba walichaguliwa kuendelea baada ya mchujo wa awali.”
Aliongeza kuwa baada ya usaili uliofanywa na Kamati ya Mkutano wa Makatibu Wakuu wa nchi wanachama, Dkt. Kapologwe alipata alama za juu zaidi na kuingia katika hatua ya mwisho pamoja na wagombea wengine wawili kutoka Kenya na Malawi.
"Majina yao matatu yaliwasilishwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati, na Kusini (ECSA – HC), ambapo Dkt. Kapologwe ameibuka mshindi," alisema Mhagama.
Kwa ushindi huu, Tanzania inaendelea kuthibitisha kuwa ina wataalam wenye sifa za kushika nafasi za uongozi katika jumuiya na mashirika ya kimataifa, huku ikichangia kuboresha huduma za afya kwa mataifa mbalimbali.
Jumuiya ya ECSA-HC ilianzishwa mwaka 1974 na inajumuisha nchi wanachama tisa: Tanzania, Malawi, Kenya, Lesotho, Zambia, Zimbabwe, Mauritius, Uganda, na Eswatini. Pia, inashirikiana na nchi 13 zisizo wanachama, zikiwemo Botswana, Burundi, Cameroon, Eritrea, Gabon, Liberia, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Seychelles, Sudan ya Kusini, Sudan, na Somalia.
Kufuatia ushindi huo, wajumbe wa Tanzania walishangilia huku wakimpongeza mgombea wao aliyependekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwania nafasi hiyo.
0 Comments:
Post a Comment