Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2025 yanatarajiwa kuwa ya kipekee, kwani yataambatana na kumbukumbu ya miaka 30 ya utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing la mwaka 1995.
Haya yamebainika jijini Dar es Salaam tarehe 3 Februari 2025, wakati wa mkutano wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo.
Maadhimisho Kufanyika Kitaifa Mkoani Arusha
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Dkt. Gwajima alieleza kuwa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi 2025 kitafanyika kitaifa mkoani Arusha. Kabla ya siku hiyo, maadhimisho yatafanyika katika ngazi ya mikoa ili kuwezesha ushiriki mpana wa wanawake na jamii kwa ujumla.
"Katika mkutano huo wa Beijing yalifikiwa maazimio ambayo Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa imeendelea kutekeleza. Mwaka huu ni wa thelathini tangu utekelezaji ulipoanza, hivyo mataifa yatatumia maadhimisho haya kutathmini utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing na kuweka mikakati endelevu," alisema Dkt. Gwajima.
Alibainisha kuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kaulimbiu ya Mwaka 2025
Dkt. Gwajima alieleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”, ambayo inatokana na kaulimbiu ya kimataifa “For All Women and Girls. Equality. Rights. Empowerment”.
"Lengo la kaulimbiu hii ni kuhamasisha jamii kukuza usawa wa kijinsia, haki na uwezeshaji wa wanawake na wasichana. Pia, tunalenga kuwaandaa wanawake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025 ili wajiamini, wajiandae na wajitokeze kugombea nafasi za uongozi," alisisitiza Dkt. Gwajima.
Huduma na Maonesho kwa Wananchi
Waziri alifafanua kuwa katika wiki ya maadhimisho, taasisi za umma, binafsi na makampuni zitatoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Aidha, kutakuwa na maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wa kike.
"Natoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo yao kupata huduma na kununua bidhaa mbalimbali za wajasiriamali, ili kuwaunga mkono wanawake katika kujikwamua kiuchumi," alisema Dkt. Gwajima.
Sare Maalum ya Kitaifa
Alitangaza kuwa kwa kushirikiana na wadau, Wizara imeandaa sare maalum ya kitaifa kwa ajili ya siku ya kilele cha maadhimisho, ambayo ni kitenge kitakachopatikana kwa bei ya kati ya TSh 25,000 hadi 30,000, kutegemeana na eneo.
"Kabla ya kilele cha maadhimisho, kila mkoa utaadhimisha kwa kutumia sare zao, lakini kwa siku ya kitaifa, sare hii maalum itatumika," alieleza.
Maadhimisho ya Kipekee
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, alisema kuwa mwaka huu maadhimisho yatakuwa ya kipekee kwa sababu huadhimishwa kitaifa kila baada ya miaka mitano.
"Kutakuwa na mijadala, makongamano na huduma mbalimbali kwa wananchi, sambamba na elimu juu ya masuala ya uwezeshaji wanawake na usawa wa kijinsia," alisema Dkt. Jingu.
Arusha Kuchaguliwa Ili Kupaza Sauti Dhidi ya Mila Kandamizi
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdulnoor, alisema kuwa Serikali imeamua kufanya maadhimisho hayo kitaifa mkoani Arusha ili kusaidia kupaza sauti dhidi ya mila kandamizi zinazomrudisha nyuma mwanamke na mtoto wa kike.
"Tunataka kutumia fursa hii kuhamasisha jamii ya Arusha na mikoa jirani kuachana na mila zisizofaa, na pia kuwahimiza wanaume kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau katika kupigania usawa wa kijinsia nchini," alisema Abdulnoor.
Serikali inawahimiza wananchi wote, hususan wanawake, kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kwa kushiriki uzinduzi, maonesho, na makongamano, ili kuhakikisha kuwa yana tija kwa maendeleo ya wanawake nchini Tanzania.




0 Comments:
Post a Comment