Maboresho ya Miundombinu Yachochea Ongezeko la Watalii Hifadhi ya Taifa Saadani

 


Hifadhi ya Taifa Saadani imeendelea kushuhudia mafanikio makubwa katika kuongeza idadi ya watalii, huku miundombinu iliyoboreshwa ikiwa na mchango mkubwa katika maendeleo hayo. 



Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Musa Nassoro Kuji, alishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa juhudi za kuboresha miundombinu, ikiwemo barabara na uwanja wa ndege, hatua ambayo imeongeza idadi ya wageni na mapato katika hifadhi hiyo. 



Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 01 Februari 2025, Kamishna Kuji alisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya juhudi za pamoja za maafisa na askari wa hifadhi katika kutekeleza majukumu yao.



Kamishna Kuji alifafanua kwamba, ongezeko la wageni katika Hifadhi ya Taifa Saadani limeongezeka kwa zaidi ya asilimia kumi na saba, jambo linaloashiria mafanikio ya utekelezaji wa mipango ya Serikali. 


“Nimepokea taarifa ya Saadani kuna ongezeko la watalii zaidi ya asilimia kumi na saba. Mafanikio haya yamepelekea kuongezeka kwa mapato kufikia bilioni 1.7, ikiwa ni makusanyo ya miezi saba. 


Makadirio yetu ni kufikia bilioni mbili kwa mwaka katika Hifadhi hii,” alisema Kamishna Kuji.


Aliongeza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya mchango wa kila hifadhi, ambapo TANAPA imejipanga kutoka katika kukusanya bilioni hadi kufikia trilioni. 


“Mafanikio haya ya TANAPA ni matokeo ya mchango wa kila hifadhi ili kufikia lengo kuu la Serikali katika kuhifadhi na kuongeza mapato,” alisisitiza Kamishna Kuji.



Afisa Uhifadhi Mkuu na Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani, Gladys Ng’umbi, alieleza kuwa maboresho makubwa ya miundombinu katika hifadhi hiyo yamechochea ongezeko kubwa la watalii. 


Alitaja baadhi ya maboresho yaliyofanyika, ikiwa ni pamoja na ongezeko la urefu wa uwanja wa ndege wa Saadani kufikia kilometa 1.4 kutoka 1.0 na ukarabati wa barabara za utalii zenye urefu wa kilomita 74. Aidha, barabara mpya za utalii zenye urefu wa kilomita 6.5 zimefunguliwa.



Ng’umbi alifafanua kuwa hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza urahisi wa usafiri na kupunguza changamoto za kufika kwa watalii katika hifadhi hiyo. 


“Maboresho haya ya miundombinu yamekuwa na manufaa makubwa, kwani sasa watalii wanaweza kufika kwa urahisi na kwa haraka,” alisema Ng’umbi.


Hifadhi ya Taifa Saadani pia imejipanga kushirikiana na taasisi nyingine, kama vile Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuongeza idadi ya watalii kwa kutumia njia ya reli kutoka Dar es Salaam hadi Arusha. 


“Hadi sasa, tumeshafanya upembuzi yakinifu wa eneo la ujenzi wa gati (maegesho ya boti) ya kushushia wageni wanaotoka Zanzibar na Tanga kwa njia ya boti,” alisema Ng’umbi.


Pia, alitoa rai kwa wawekezaji kuchangamkia fursa za uwekezaji katika utalii wa maji, akibainisha kwamba Hifadhi ya Taifa Saadani ina fursa nyingi katika sekta ya utalii wa kwenye maji (Blue Tourism). 


“Tunatoa rai kwa wawekezaji kuchangamkia fursa za uwekezaji katika maeneo ya utalii wa maji, kwani kuna uhitaji mkubwa wa miundombinu bora ya kusafirisha watalii kwa njia ya boti,” aliongeza.



Kwa jumla, mafanikio yaliyopatikana katika Hifadhi ya Taifa Saadani ni sehemu ya juhudi kubwa zinazofanywa na TANAPA na Serikali kwa ujumla katika kuboresha miundombinu ya utalii na kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii, ambayo ni moja ya vyanzo vikuu vya uchumi nchini. 


Maboresho haya yanaonyesha mafanikio ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, taasisi mbalimbali na sekta binafsi katika kukuza sekta ya utalii na kuhakikisha hifadhi za taifa zinaendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

0 Comments:

Post a Comment