Serikali ya Tanzania inaendelea kubuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, huku ikijiandaa kupitia upya kanuni za malipo ya kifuta jasho na machozi kwa waathirika.
Katika ziara yake mkoani Tanga, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali inaongeza askari wanyamapori na kutumia teknolojia za kisasa kama ndege zisizo na rubani (drones) kudhibiti wanyama waharibifu.
"Tunaendelea kuongeza askari wanyamapori na kubuni mbinu mbalimbali za kufukuza wanyama, ikiwemo kutumia ndegenyuki (drones)," alisema Rais Samia wakati wa mkutano wake na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa chama na serikali, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, Naibu Waziri Dunstan Kitandula, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, pamoja na watendaji kutoka taasisi za wizara hiyo.
Ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji Mkomazi Kuanza Rasmi
Katika muendelezo wa ziara yake mkoani Tanga, Rais Samia ameweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Mkomazi wilayani Korogwe, akisema kuwa hatua hiyo inatimiza ndoto ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ya kuboresha sekta ya kilimo nchini.
Bwawa hilo linatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakazi 20,000 wa wilaya hiyo kwa kuwawezesha wakulima kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka bila kutegemea mvua.
"Dhamira ya serikali ni kumuinua mkulima kwa kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo," alisema Rais Samia.
Bwawa hilo litakuwa na tuta lenye urefu wa zaidi ya mita 300, barabara za mashambani zaidi ya kilomita 56, na litaweza kuhifadhi lita bilioni 17 za maji. Ujenzi wake unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 48 na utahusisha zaidi ya kata 20 wilayani Korogwe.
Akielezea mradi huo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema kuwa serikali kwa miaka mingi imekuwa na changamoto za kulitekeleza bwawa hilo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo masuala ya kisiasa na kifedha. Hata hivyo, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejidhatiti kuhakikisha mradi huo unakamilika.
"Serikali inalenga kuwavutia wawekezaji wakubwa wa mazao mengine kama vile kilimo cha chai, ili kutoa fursa kwa wakulima kupata nafasi ya kuuza mazao yao kwenye soko la ndani na nje ya nchi," alisema Bashe.
Hatua hii ya serikali inaashiria mwamko mpya katika kuboresha kilimo na usalama wa wananchi dhidi ya wanyamapori wakali, ikiwa ni juhudi za kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla.







0 Comments:
Post a Comment