NCAA NA KAMPUNI YA TANZANITE COORPORATES WAANDAA SAFARI MAALUMU YA WANAWAKE NGORONGORO KUELEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

 


Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na kampuni ya Tanzanite Cooperate imeandaa safari maalumu ya siku moja (Day Trip) kwa wanawake ili kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi ya Ngorongoro, hususan Kreta ya Ngorongoro, kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.



Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia huduma za Utalii NCAA, Mariam Kobelo, alisema safari hiyo inalenga kuwahamasisha wanawake kushiriki katika utalii wa ndani kama sehemu ya kuenzi juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutangaza vivutio vya utalii nchini.



"Kama mnavyojua, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara wa kutangaza utalii wetu kupitia filamu za Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania. Sisi kama wanawake wa sekta ya utalii tumeamua kumuunga mkono kwa kuhamasisha wanawake kushiriki safari hii ya Ngorongoro.


Tunawahakikishia watakaolipia kifurushi cha shilingi 170,000 watapata uzoefu wa kipekee wa utalii (unforgettable experience)," alisema Kobelo.



Kwa mujibu wa Kobelo, safari hiyo itafanyika Machi 7, 2025, ambapo washiriki wataondoka jijini Arusha saa 11 alfajiri kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na kurejea jioni hiyo hiyo. Safari hiyo itajumuisha gharama za kiingilio, chai ya asubuhi, chakula cha mchana, usafiri, gharama za muongoza watalii, pamoja na kila mshiriki kupewa kofia atakayovaa wakati wa safari.


"Kwa wote watakaoshiriki safari hii, wanatarajia kushuhudia vivutio mbalimbali vya asili, wanyamapori wakiwemo 'Big Five' (simba, chui, faru, tembo, na nyati), pamoja na mandhari ya kuvutia ya Kreta ya Ngorongoro, ambayo ni moja ya maajabu saba ya Afrika," aliongeza Kobelo.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tanzanite Cooperate, Elina Mwangomo, aliwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kushiriki safari hii ili kuunga mkono jitihada za utalii wa ndani.



"Tunapenda kuwakaribisha wanawake wote kushiriki safari hii ili kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani kwa namna ya kipekee. Kwa yeyote anayependa kushiriki, tafadhali wasiliana nasi kupitia namba 0758 171 914 au 0763 291 179 kwa maelekezo zaidi ya malipo na usajili," alisema Mwangomo.



Aidha, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu yatafanyika kitaifa jijini Arusha Machi 8, 2025, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Wanawake walioko katika sekta ya utalii wanatarajia kushiriki maadhimisho hayo kwa wingi ili kutambua mchango wa wanawake katika uhifadhi na utalii nchini.


Kwa upande wake mwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Thabea Mollel amewahakikishia wanawake wote watakaoshiriki safari ya utalii Ngorongoro watapata usalama wa hali juu katika safari ya utalii katika hifadhi ya Ngorongoro na kurudi Arusha.

"WANAWAKE NA UTALII, TAMBUA MCHANGO WA MWANAMKE KATIKA SEKTA YA UHIFADHI NA UTALII. TUMERITHISHWA, TUWARITHISHE."

0 Comments:

Post a Comment