Maji Yakatiza Tuzo za Trace Afrika Zanzibar, Rema Ang'ara

 


Tuzo za muziki za Trace Afrika, zilizofanyika kwa mara ya kwanza Visiwani Zanzibar, Tanzania, usiku wa kuamkia leo, zilikatizwa ghafla baada ya maji kujaa karibu na jukwaa, hali iliyosababisha sintofahamu kwa mashabiki na wageni waalikwa.


Tamasha hilo lilianza kwa kuchelewa kutokana na upepo mkali na mawimbi, na waandaaji walilazimika kusogeza muda wa kuanza hadi saa 4 usiku. Msanii wa Tanzania, Marioo, alikuwa wa kwanza kutumbuiza kabla ya wasanii wengine kuendelea na burudani. Hata hivyo, shughuli hiyo ilikatizwa ghafla mnamo saa 9:20 usiku, ikiwa bado katika hatua za mwanzo za kutangaza washindi wa tuzo hizo.

Ingawa sababu rasmi haikutangazwa jukwaani, tukio hilo lilizua minong’ono na malalamiko kutoka kwa waliohudhuria. Kabla ya kusitishwa, msanii Rema kutoka Nigeria alitangazwa kuwa Msanii Bora wa Kiume wa Mwaka na pia kushinda Tuzo ya Albamu Bora kupitia albamu yake Heis.


Tuzo zingine zilimwendea P. Prime kutoka Nigeria kama Mtayarishaji Bora wa Muziki, Josey kutoka Ivory Coast kama Msanii Bora wa Nchi zinazozungumza Kifaransa, Joe Dwet File (Ufaransa/Haiti) kama Msanii Bora wa Diaspora, na Duquesa kutoka Brazil.


Licha ya changamoto hiyo, tamasha hilo lilishuhudia burudani ya nguvu kutoka kwa wasanii wakubwa wa Afrika, akiwemo Diamond Platnumz wa Tanzania, Harmonize, na Bien wa Kenya.

0 Comments:

Post a Comment