Dk. Slaa Aachiliwa Huru, Aonyesha Utayari wa Kurudi CHADEMA

 


Dar es Salaam – Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, ameonyesha utayari wa kurejea katika chama hicho cha upinzani baada ya kuachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.


Dk. Slaa alikuwa akikabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za uongo kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), lakini leo Februari 27, 2025, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alieleza kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema, aliwasilisha nia hiyo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Franco Kiswaga, kwa mujibu wa Kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kinachompa mamlaka DPP kuondoa shauri lolote mahakamani isipokuwa yale yaliyofikia hatua ya hukumu.



Baada ya kuachiwa huru, Dk. Slaa alizungumza na waandishi wa habari na kueleza msimamo wake kuhusu siasa na mustakabali wake ndani ya CHADEMA.


"Mimi nadhani kwa sababu kile tunachokipigania wamekiweka wazi. Sasa hivi kile kilichoniondoa 2015 kimeshafutika. Sina tatizo lolote kufanya kazi kwa karibu zaidi na CHADEMA kwa utaratibu wa CHADEMA," alisema Dk. Slaa.


Aliongeza kuwa yeye alikuwa mwanaharakati na ataendelea kuwa mmoja, lakini sasa yupo tayari kushirikiana na chama hicho cha upinzani kwa sababu mazingira yamebadilika.


"Mimi nilikuwa mwanaharakati, na bado ni mwanaharakati. Hakuna mtu anayeweza kuniambia nisiwe mwanaharakati. Hata nilipokuwa Vatican, nilikuwa mwanaharakati wa haki za binadamu na bado naendelea kuwa hivyo. Lakini suala la CHADEMA, kwa sasa sina tatizo nalo kabisa," alisisitiza.


Dk. Slaa alijitenga na CHADEMA mwaka 2015 baada ya kutofautiana na chama kuhusu uamuzi wa kumkaribisha Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). Sasa, baada ya zaidi ya miaka tisa, inaonekana yuko tayari kurejea kwenye siasa za upinzani.

0 Comments:

Post a Comment