WASSIRA ACHAGULIWA MAKAMU MWENYEKITI CCM BARA



Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeidhinisha uteuzi wa Stephen Wassira kuwa Makamu Mwenyekiti mpya wa chama hicho upande wa Tanzania Bara. 


Wassira anachukua nafasi ya Abdulrahman Kinana, ambaye alijiuzulu wadhifa huo, hatua ambayo iliidhinishwa na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Rais wa Tanzania.


Kinana alihudumu katika nafasi hiyo kwa takribani miaka miwili na miezi mitatu tangu kuchaguliwa kwake mwezi Aprili 2022. 


Wassira, ambaye ni mzee mwenye umri wa miaka 80, amekuwa na uzoefu mkubwa katika utawala wa serikali akiwa ameshika nafasi mbalimbali za Naibu Waziri na Waziri katika serikali ya Tanzania tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere hadi awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.


Wassira anatarajiwa kuwa nguzo muhimu ya ushauri kwa Mwenyekiti Samia, hasa katika kusimamia nidhamu ndani ya CCM wakati taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, ambapo Samia anatarajiwa kugombea kipindi cha pili na cha mwisho cha urais.


Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Bara ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili na Nidhamu ya chama hicho.

0 Comments:

Post a Comment