MBOWE AZUNGUMZA KUHUSU MAPINDUZI NA MENGINE YA SIASA ZA CHADEMA




Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameweka wazi maoni yake kuhusu madai ya baadhi ya watu kutaka kumpindua na changamoto zinazokikumba chama hicho, akisema kuwa haki itashinda na uongo hautatawala.


Akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet kilichorushwa na chaneli ya runinga ya UTV, Mbowe alisema: "Mimi watu kutaka kunipindua nimelisikia na ninalisikia, kwasababu sikuwa sehemu ya hao wanamapinduzi sijui ajenda yao walitaka kuibeba vipi! Kwahiyo nisingetamani kuingia kwenye mjadala huo, wao ukiwauliza wanaweza kuwa na majibu zaidi. Lakini dunia hii haina siri, vitu vya hila ni suala la muda tu na haki haijawahi kushindwa na uongo haujawahi kutamalaki."


Mbowe aliongeza kuwa siasa ni mchezo wa timu na kwamba, "huwezi kuwa kiongozi ambaye eti unataka kukiongoza chama kwa kuwashusha wenzio, kwa kuwakanyaga wenzako, kwa kuwatweza wenzako." Alisema kuwa katika siasa, umoja na ushirikiano ni muhimu ili kufanikisha malengo.


Akizungumzia udhaifu wa binadamu, Mwenyekiti huyo alikiri kuwa viongozi pia wanamapungufu yao. Alisema, "Sisi ni binadamu, tuna mapungufu, yawezekana Mwenyekiti Mbowe ana mapungufu yake, Katibu Mkuu wangu ana mapungufu yake halikadhalika Wajumbe wa Kamati Kuu, kila binadamu ana mapungufu yake."


Alimalizia kwa kusema kuwa licha ya changamoto wanazokutana nazo, umoja wa chama na nguvu yao ya pamoja ndiyo silaha yao kubwa katika kudai haki.

0 Comments:

Post a Comment