Samia na Mwinyi Kubeba Bendera ya CCM kwa Uchaguzi Mkuu wa 2025

 


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemteua rasmi Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kubeba bendera ya chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. 


Uamuzi huu unaonyesha imani kubwa kwa uongozi wa Rais Samia, ambaye ameonyesha mafanikio makubwa katika kipindi cha uongozi wake, ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi, miundombinu, na huduma za afya.


Katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika mjini Dodoma, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alitoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuhakikisha wanazingatia utaratibu rasmi wa chama kwa kupitisha azimio la kuidhinisha majina ya viongozi hao kama wagombea wa urais. 


Kikwete alisema, “Kama tumekubaliana katika mkutano huu, basi Rais Samia na Rais Mwinyi wanaelekea kushinda tena kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Lakini ni muhimu tupitishe azimio rasmi ili kuhakikisha tunazingatia taratibu za chama na kutoa ujumbe wa mshikamano kwa wanachama wote.”


Aidha, Kikwete alisisitiza kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao hauna shaka kutokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Samia na Mwinyi, na kuongeza kuwa, “Hatua hii ni muhimu kwa kuimarisha mshikamano ndani ya chama na kuhakikisha tunapata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.”


Kwa kumalizia hotuba yake, Kikwete aliwatia moyo wajumbe kwa kuanzisha wimbo wa kuonyesha imani kwa Rais Dk. Samia na Dk. Mwinyi, wimbo ambao ulizua shangwe kubwa katika ukumbi wa mkutano. 


Hatua hii ya Rais Mstaafu Kikwete imeonyesha uzalendo wake na umakini katika kulinda mshikamano wa CCM, huku akisisitiza umuhimu wa kuheshimu misingi ya kidemokrasia na taratibu za chama.


Kwa upande mwingine, uteuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kama mgombea urais kwa mwaka 2025, ni ishara ya kuendelea kwa mafanikio ya CCM, huku Rais Samia akijivunia mafanikio yaliyopatikana katika utawala wake, na kuahidi kuwa chama hicho kitendelea kutoa maendeleo kwa wananchi.

0 Comments:

Post a Comment