Marekani imetangaza kusitisha mpango wa ushuru kwa bidhaa za Colombia baada ya Bogota kukubali kupokea wahamiaji waliofukuzwa kutoka Marekani bila vikwazo vyovyote.
Haya yanajiri baada ya mzozo wa kidiplomasia uliosababishwa na hatua ya awali ya Colombia kuzuia ndege za kijeshi za Marekani zilizokuwa zimebeba wahamiaji kutua nchini humo.
Ikulu ya Marekani, White House, imethibitisha kuwa serikali ya Colombia sasa imekubali kupokea wahamiaji kupitia ndege za kijeshi za Marekani "bila kikomo au kuchelewa."
Taarifa hiyo pia imebainisha kuwa mazungumzo zaidi yataendelea ili kuhakikisha utu na heshima ya wahamiaji wa Colombia wanaorudishwa nyumbani.
Awali, Rais wa Colombia Gustavo Petro alitangaza kuwa nchi yake haitaruhusu ndege za kijeshi za Marekani kutua na badala yake akasema, "Tutawapokea raia wenzetu kwenye ndege za kiraia, bila kuwachukulia kama wahalifu."
Hata hivyo, hatua hiyo ilisababisha mvutano mkubwa, huku Rais wa Marekani Donald Trump akijibu kwa vitisho vya kiuchumi.
Trump alitangaza kwamba Marekani ingeweka ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa zote kutoka Colombia na kuongeza kwamba ushuru huo ungepanda hadi asilimia 50 ndani ya wiki moja.
"Hatua hizi ni mwanzo tu," alisema Trump, akiongeza kuwa serikali yake haitaruhusu Colombia
"kukwepa majukumu yake ya kisheria kuhusiana na kurudi kwa wahalifu waliowalazimisha nchini Marekani."
Colombia pia ilijibu kwa vikali kupitia Rais Petro, ambaye alitangaza ushuru wa kulipiza kisasi wa asilimia 25 kwa bidhaa za Marekani.
"Tutajibu kwa heshima na nguvu," Petro aliandika katika mtandao wa X (zamani Twitter), akiongeza kuwa Colombia ni nchi yenye ujasiri wa kupinga shinikizo lolote.
Licha ya msimamo wa awali wa Colombia, hali ilibadilika baada ya mazungumzo ya kidiplomasia.
Hatimaye, Bogota ilikubali kuruhusu ndege za kijeshi za Marekani kuwasilisha wahamiaji waliofukuzwa, hatua iliyosababisha kusitishwa kwa ushuru uliokuwa umetangazwa na Marekani.
Serikali ya Colombia imesema kuwa mazungumzo zaidi yataendelea ili kuhakikisha kuwa raia wake wanarudishwa kwa "utu na heshima."



0 Comments:
Post a Comment