Jaji Merchan Kutoa Hukumu dhidi ya Trump Kabla ya Kuapishwa

 


Jaji wa Mahakama ya New York, Juan Merchan, ambaye anasikiliza kesi ya utoaji hongo dhidi ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump, anatarajiwa kutoa uamuzi juu ya kesi hiyo siku 10 kabla ya kuapishwa kwake Januari 20, 2024.


Jaji Merchan amesema kuwa Trump, ambaye ni rais wa kwanza wa zamani kuwahi kuhukumiwa kwa uhalifu, anaweza kujitokeza ana kwa ana au kwa njia ya mtandao wakati hukumu yake itakaposomwa tarehe 10 Januari, 2024.


Katika uamuzi wa kurasa 18, Merchan alikataa hoja mbalimbali za mawakili wa Trump waliotaka hukumu hiyo itupiliwe mbali. 


Jaji huyo pia alibainisha kwamba hana nia ya kutoa adhabu ya kifungo jela, badala yake anategemea kuachiliwa bila masharti, huku hukumu nyepesi ikimfanya Trump kuwa rais wa Marekani aliye na hatia ya uhalifu. Hata hivyo, Trump anatarajiwa kukata rufaa, ambayo inaweza kuchelewesha hukumu yake.


Trump alipatikana na hatia katika kesi ya makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara ili kuficha malipo kwa nyota wa filamu za ngono, Stormy Daniels, kabla ya uchaguzi wa rais wa 2016. 


Mawakili wa Trump walijaribu kupinga kesi hiyo kwa kudai kuwa marais wa zamani wana kinga ya kutoshtakiwa kwa vitendo vya kiofisi. Hata hivyo, Jaji Merchan alikataa hoja hiyo, akisisitiza kwamba Trump hataweza kushtakiwa mara tu atakapoapishwa tena kama rais.


Msemaji wa Trump, Steven Cheung, alielezea hasira kuhusu uamuzi wa Jaji Merchan, akisema: "Kesi hii ya uvunjaji sheria haikupaswa kamwe kuletwa na Katiba inataka itupiliwe mbali mara moja."


Trump pia anakabiliwa na kesi mbili za shirikisho zinazohusiana na uchaguzi wa 2020 na uondoaji wa nyaraka za siri baada ya kuondoka Ikulu ya Marekani. Hata hivyo, kesi hizo zilitupiliwa mbali kwa misingi ya sera ya muda mrefu ya kutomshtaki rais aliyekuwa madarakani.

0 Comments:

Post a Comment