Na Gift Mongi
Moshi
Ikiwa ni dakika za lala salama kupelekea uchaguzi wa serikali za mitaa hapo novemba 27 2024 mbunge wa jimbo la Moshi Vijijini Prof Patrick Ndakidemi na yule wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro Zuwena Bushiri wamewasihi wananchi wote wa Kata ya Mabogini iliyoko katika Jimbo la Moshi Vijijini kuwachagua viongozi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Wabunge hawa walisema, CCM inauzika nchi nzima kutokana na kazi nyingi na nzuri zinavyofanywa na madiwani, Wabunge na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mabogini eneo la Ubungo huko Shabaha na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, Ndakidemi na Zuwena Bushiri waliwatambulisha wagombea ambao ni Wenyeviti wa Serikali za Vijiji, Vitongojji na Wajumbe wa Halmashauri za Vijiji wanaogombea kupitia CCM na kuwaambia akina Baba, Wamama na Vijana kuwa hawatajuta hata kidogo kuichagua CCM.
Wazungumzaji wengi waliopata fursa ya kuzungumza walielezea maendeleo yaliyoletwa Mabogini na Serikali ya CCM katika Kata hiyo. Kwa mfano, upatikanaji wa maji safi na salama ya bomba imeweka historia kwani kuna maeneo ya Mabogini ambayo tokea Tanzania ipate uhuru yalikuwa hayajafikiwa na maji ya bomba.
Akina mama walikuwa wanasafiri umbali mrefu kuyatafuta maji. Miradi mingine iliyotekelezwa na serikali ya CCM ni pamoja na kuanza kwa ujenzi wa barabara ya lami kutokea Zara - Mabogini - Kahe, Ujenzi wa hospitali ya Wilaya na Zahanati ya Mvuleni, Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Mtakuja, kuchimba visima viwili vya maji ya kunywa, kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali ya Kata ya Mabogini, ujenzi wa madarasa katika shule zote za Sekondari na baadhi ya Shule za Msingi, ujenzi wa mnara wa mawasiliano ya simu na miradi mingine mingi.
Wananchi walijulishwa kwamba, kwa ujumla, katika kipindi cha miaka minne, Kata ya Mabogini imepokea miradi yenye thamani ya zaidi ya TZS bilioni nane kutokana na juhudi za viongozi wa serikali za Vijiji, Diwani na Mbunge.
Kutokana na mafanikio hayo ya muda mfupi, Mbunge Ndakidemi aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura za ndiyo za kishindo ili wagombea wanaotokana na CCM washinde na wao ndio watakuwa daraja la kuzichukua kero zao na kuzifikisha kwenye mamlaka husika.
0 Comments:
Post a Comment