Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imebaini kuwepo kwa majukwaa na programu tumizi 69 zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kidijitali bila leseni wala idhini kutoka Benki Kuu.
Akizungumza kupitia taarifa rasmi iliyotolewa Novemba 21, 2024, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, amesema hatua hiyo inalenga kulinda wananchi dhidi ya huduma za kifedha zisizokidhi viwango vinavyotakiwa.
“Programu hizi hazijakidhi matakwa ya Mwongozo wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili unaosimamia utoaji wa mikopo kwa njia ya kidijitali.
Mwongozo huu unazingatia uwazi, uadilifu, na ulinzi wa faragha za wateja,” alisema Gavana Tutuba.
Aidha, BoT imeeleza kuwa inashirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzifungia programu hizo ili kuzuia wananchi kuendelea kutumia huduma zisizokuwa na vibali vya kisheria.
Miongoni mwa programu zilizotajwa katika orodha hiyo ni pamoja na BoBa Cash, BongoPesa, Mkopofast, Tala, Viva Mikopo Limited, Yes Pesa, na ZimaCash.
Benki Kuu imewataka wananchi kutojihusisha na majukwaa hayo na badala yake kutumia huduma za kifedha kutoka kwa watoa huduma walioidhinishwa.
“Benki Kuu imechapisha na itaendelea kuhuisha orodha ya watoa huduma halali katika tovuti yake rasmi,” aliongeza Gavana Tutuba.
Kwa taarifa zaidi, wananchi wanahimizwa kuwasiliana na Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania kupitia simu +255 22 223 5586 au barua pepe info@bot.go.tz.
Taarifa kamili na orodha ya majukwaa yasiyo halali inapatikana kwenye tovuti ya BoT: [www.bot.go.tz](https://www.bot.go.tz).
0 Comments:
Post a Comment