Askofu Shoo Ahimiza Ushirikiano wa KKKT na Serikali, Rais Samia Atoa Shilingi Milioni 20 kwa Askofu Massangwa

 


Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Fredrick Shoo, amesema kanisa hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya awamu ya sita katika kupinga uminyaji wa haki za watu pamoja na imani za kishirikina nchini Tanzania, ambazo zimesababisha watu wengi kutopea kwenye umaskini. 


Akizungumza Jumapili, Septemba 29, 2024, katika ibada maalum ya kumstaafisha kwa heshima Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dkt. Solomon Massangwa, Dkt. Shoo alisema, “Tunaona mambo mengi na balaa nyingi zimekuja katika nchi hii kwa sababu wapo hata viongozi wa ngazi za juu sana wanashiriki katika mambo hayo kwa sababu ya imani zao kuwatuma wakati wa kutafuta vyeo. 


Ni wajibu wetu wa viongozi wa dini kushirikiana na viongozi wa serikali kukemea mambo hayo.”



Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kimandolu, Jijini Arusha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alitoa zawadi ya Shilingi milioni 20 kwa Askofu Dkt. Massangwa kama ishara ya shukrani kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa amani na mshikamano ndani ya mkoa huo. 



“Baba Askofu Massangwa ni miongoni mwa maaskofu waliojenga amani, umoja na mshikamano katika Mkoa wetu wa Arusha,” alisema Makonda.


Aidha, Makonda aliwakumbusha waumini wa KKKT umuhimu wa kuwatunza viongozi wastaafu wa kanisa hilo, akisema, “Ipo tabia ambayo ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu ya makanisa na waumini wa dini ya Kikristo kuwasahau viongozi wao pindi wanapostaafu.”



Askofu Dkt. Solomon Massangwa, ambaye amehudumu kwa zaidi ya miaka 42 ndani ya kanisa hilo, amepongezwa kwa kazi yake kubwa ya kulipa madeni ya kanisa, kuboresha elimu kwa wachungaji wapya, na kuimarisha huduma za ibada kwa kuongeza wataalamu wa muziki ndani ya dayosisi hiyo.

0 Comments:

Post a Comment