Waasi wa M23 Wauteka Mji wa Kanyabayonga Mashariki mwa DRC
Waasi wa M23 wameuteka mji wa kimkakati wa Kanyabayonga mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mapema Jumamosi baada ya mapigano makali na vikosi vya Congo.
Waasi hao walichukua udhibiti wa maeneo mawili kabla ya kuuteka Kanyabayonga, mji muhimu ulioko kati ya vituo vikuu vya kibiashara vya Butembo na Beni kaskazini mwa nchi hiyo.
Afisa mmoja wa eneo hilo aliripoti kuwa wakazi walikimbia makazi yao mwendo wa alfajiri wakati waasi wakianzisha mashambulizi yao.
Kanyabayonga imekuwa kimbilio la maelfu ya watu ambao wamekimbia kutoka kwa waasi katika miezi ya hivi karibuni.
Mkoa wa Kivu Kaskazini umekumbwa na ghasia tangu 2021, wakati M23 walipoanzisha tena mashambulizi yao.
Kinshasa imefutilia mbali mazungumzo yoyote na M23. Kwa pamoja na Umoja wa Mataifa, inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi, madai ambayo Kigali inakanusha.
0 Comments:
Post a Comment