TANAPA Yazindua Mpango wa Geo-Park kwa Ajili ya Kutangaza Vivutio vya Asili na Kuwanufaisha Wananchi

 TANAPA Yazindua Mpango wa Geo-Park kwa Ajili ya Kutangaza Vivutio vya Asili na Kuwanufaisha Wananchi


Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA), kupitia Hifadhi ya Arusha (ANAPA), limeanzisha mpango kabambe wa kuvitangaza vivutio vya asili vilivyoko ndani na nje ya hifadhi hiyo ili viweze kuwanufaisha wananchi wanaozunguka hifadhi. Mpango huu unajulikana kama Geo-Park.



Kamanda wa Hifadhi ya ANAPA, Yustina Kiwango, amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya asili, lakini vingi kati ya hivyo vinajulikana kupitia hifadhi za taifa pekee, huku vingine vikikosa kutambulika na wananchi wa kawaida. 


"Vivutio hivi ambavyo vinatokana na sababu za kijiolojia tangu enzi za mababu, wananchi wakielekezwa jinsi ya kuvilinda, kuvitunza na kuvitumia kibiashara, vitawaingizia vipato vya kutosha kubadilisha maisha yao," alisema Kiwango.


Kiwango aliongeza kuwa katika wilaya ya Arumeru pekee, kuna zaidi ya vivutio 16 vya asili vilivyotokana na volkeno na mabadiliko ya kiokolojia. Miongoni mwa vivutio hivyo ni maporomoko ya maji marefu sana yaliyopo katika kijiji cha Bangata, Ziwa Duluti lililoko Tengeru, na Mto Njiku ambao ulikuwa unatumika na mababu wa Kimeru kama sehemu ya kuondoa mikosi.


Vivutio vingine ni pamoja na mti mkubwa wa siku nyingi unaoaminika kutibu magonjwa mengi, jiwe la moyo lililotumika kama sehemu ya kupeana moyo wakati wa ujenzi wa shule ya Kisimiri, na maeneo mengine yenye historia ya kipekee.


Kamanda Kiwango aliwataka wananchi wa wilaya ya Arumeru kupokea vizuri mradi huo wa Geo-Park kwani utawanufaisha wao wenyewe, huku ANAPA ikijitolea kutoa ushauri wa kiufundi. Naye Afisa Uhifadhi wa ANAPA, Jerome Ndanzi, alielezea vivutio vingine ndani ya hifadhi ya Arusha, ikiwemo Mlima Meru wenye vilele viwili, maziwa matano yenye maji tofauti, ndege aina ya flamingo, kreta ndogo yenye wanyama muda wote, na maporomoko ya maji.



Ndani ya hifadhi hiyo pia kuna mbuyu mkubwa ambao magari yanapita katikati yake, nyani zeruzeru wanaolindwa na wenzao, na nyani aina ya mbega. 



Aidha, kuna kikundi cha wanawake kinachoitwa Umangu kilichopo kijiji cha Ngurudoto, ambacho kimepatiwa mizinga 150 ya nyuki na kinaendelea vizuri. Kikundi hiki kimepata mafanikio makubwa, ikiwemo kutembelea nchi mbalimbali kama Italia, Kenya, na Uganda kuonyesha bidhaa zao.





Kiongozi wa kikundi hicho, Sara Mwakibani, alisimulia jinsi walivyofanikiwa kwenda Italia na kuonyesha bidhaa zao licha ya changamoto za lugha, na jinsi walivyofurahia kupanda ndege kwa mara ya kwanza.


Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Emanuela Kaganda, aliwataka wananchi wa wilaya yake kupokea Geo-Park kama kichocheo cha maendeleo na kuacha kupinga mambo mema yanayofanywa na hifadhi za taifa. Alisema, "Geo-Park inakazi kubwa ya kufungua utalii nchini hasa katika wilaya yetu. Arumeru bado kuna mambo mengi ya vivutio kama makaburi ya wamisionari wa kwanza waliouawa wakitangaza injili."


Kaganda aliwataka wananchi kushirikiana vyema na hifadhi za taifa kutunza mazingira ili kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kutangaza utalii wa Tanzania duniani.



0 Comments:

Post a Comment