DC Tanganyika Afikishwa Mbele ya Baraza la Maadili Kwa Madai ya Ukiukwaji wa Maadili

DC Tanganyika Afikishwa Mbele ya Baraza la Maadili Kwa Madai ya Ukiukwaji wa Maadili



Mkuu wa wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Onesmo Mpuya Buswelu, alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili tarehe 4 Juni, 2024 kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


Buswelu anatuhumiwa kwa makosa mawili ikiwa ni pamoja na matumizi ya lugha chafu dhidi ya watumishi wa umma na kukamata watu na kuwaweka ndani bila kufuata sheria.



Kikao cha kusikiliza tuhuma dhidi ya kiongozi huyo kimefanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma chini ya uenyekiti wa  Jaji (Mst.) Rose Teemba na mjumbe wa Baraza hilo Bw. Peter Ilomo.


Wakili wa Serikali, Hassan Mayunga, aliiambia Baraza kuwa mlalamikiwa amekuwa akitumia lugha chafu na matusi kwa watumishi na watendaji wa serikali katika wilaya ya Tanganyika kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


Mayunga alisema, “Mlalamikiwa amekuwa akiwakamata na kuwaweka mahabusu wananchi na watumishi wa umma wa wilaya ya Tanganyika bila kufuata taratibu za kisheria."


Upande wa mlalamikaji ulileta mashahidi watatu ambao walieleza kuhusu matumizi ya lugha ya matusi na kukamatwa kwa watu bila kufuata sheria na taratibu.


Mlalamikiwa, ambaye ni mkuu wa wilaya ya Tanganyika, ameyakana mashtaka yote mawili na kudai kuwa anasimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya yake.


Baada ya kusikiliza pande zote mbili, Mwenyekiti wa Baraza alimueleza mlalamikiwa kuwa, “tumesikiliza pande zote, sasa liachieni Baraza lifanye upekuzi na tathmini kama kutakuwa na chochote mamlaka itakujulisha."

0 Comments:

Post a Comment