Askofu Maasa Atetea Amani Nchini: Ubovu wa Barabara Wazua Changamoto Sakila





KATIBU wa Jukwaa la Maridhiano Nchini, Askofu Dkt. Israil Maasa, ametoa kauli kali kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini Tanzania huku akisisitiza kwamba hakuna shida na namna ya kuabudu, lakini tatizo liko kwa yeyote atakayetumia imani yake kuvuruga amani ya nchi.

 


Akizungumza wakati wa mahafali ya chuo cha Biblia Sakila kinachomilikiwa na Kanisa la International Evangelism Church (IEC), ambapo zaidi ya wainjilisti, wachungaji, na maaskofu 10,000 wamehitimu.



"Mvurugaji yeyote wa amani ya Tanzania ikiwa atatoka upande wetu Wakristo huyo hakubaliki ikiwa atatoka upande wa Waislam huyo hakubaliki ikiwa atatoka upande wa mila na desturi za Kitanzania huyo hakubaliki kwa sababu amani ya Tanzania ndiyo inatufanya tuwe Watanzania na tuishi vizuri kwa pamoja na Umoja," alisema Askofu Maasa na kuongeza 


Kama mtendaji mkuu wa shughuli za jumuiya ya maridhiano, nichukue nafasi hii kuipongeza IEC kwa kuwa wadau wakubwa wa amani nchini Tanzania," .




Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa IEC, Dk. Elihudi Issangya, amesisitiza umuhimu wa kuwaombea viongozi kwa ustawi wa Taifa.


 Amesema kuwa sala na maombi ni muhimu kwa kudumisha amani nchini, na kuzingatia mafundisho ya vitabu vitakatifu.


Kanisa la IEC limeelezwa kuwa moja ya taasisi zinazoungana na serikali katika kuleta maendeleo na utulivu nchini.


Hata hivyo, wanachuo wa chuo cha Biblia Sakila wametoa malalamiko yao kuhusu ubovu wa barabara kutoka Kikatiti mpaka chuoni Sakila yenye urefu wa kilometa sita.


 Ubovu  huo wa barabara umesababisha changamoto za usafiri kwa wanafunzi na wakazi wa eneo hilo, na kuongeza gharama za uendeshaji wa chuo, hasa wakati wa kupeleka wanafunzi kwenye mafunzo ya vitendo.



Awali mwezi Juni mwaka jana, Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, aliagiza uongozi wa TARURA kuhakikisha wanatekeleza ahadi za ujenzi wa barabara ya kilometa sita kutoka Kikatiti mpaka Sakila wilayani Arumeru.


 Ahadi hizo zilitolewa kwa nyakati tofauti na Marais wa awamu mbili tofauti, John Magufuli na Samia Suluhu Hassan, wakati waliposimama kusalimia wananchi kwenye eneo la Kikatiti. 


Majaliwa alitoa agizo hilo wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye jubilee ya miaka 40 ya chuo cha Biblia Sakila kilichomilikiwa na Kanisa la International Evangelism Church (IEC). 


Alisisitiza umuhimu wa maendeleo na mchango wa Askofu Mkuu wa IEC, Dkt. Elihudi Issangya, katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye mikoa ya Arusha na Manyara.


 Chuo hicho cha Biblia Sakila kimetoa mafunzo kwa watumishi zaidi ya elfu 10 na kina malengo ya kujenga Chuo Kikuu na kuboresha zahanati ya Sakila kuwa hospitali. 


IEC pia imejenga miundombinu ya elimu na afya katika maeneo mbalimbali, na kushughulikia changamoto za maji kwenye maeneo mengi, lakini inakabiliwa na  ubovu wa barabara kutoka barabara  kuu ya  Moshi Arusha mpaka chuoni hapo.


0 Comments:

Post a Comment