Dhahabu ya Mabilioni ya Dola Yasafirishwa Kimagendo Kutoka Afrika Kila Mwaka

 Dhahabu ya Mabilioni ya Dola Yasafirishwa Kimagendo Kutoka Afrika Kila Mwaka



Ripoti mpya inayotolewa na shirika la Swissaid imebaini kuwa dhahabu yenye thamani ya mabilioni ya dola inasafirishwa kimagendo kutoka Afrika kila mwaka, huku sehemu kubwa ikielekea Umoja wa Falme za Kiarabu.


Uchunguzi huo umegundua kuwa Dubai, mji ambao unatambulika kwa soko kubwa la dhahabu, ni kituo kikuu cha kuingiza dhahabu hiyo kutoka Afrika, kabla ya kusafirishwa kwenda nchi za Ulaya kama Uswisi, India, na hata Marekani.


Mali, Zimbabwe, na Ivory Coast zimebainika kuwa ni miongoni mwa nchi zenye uzalishaji mkubwa wa dhahabu ambayo haisajiliwi rasmi. Inakadiriwa kuwa takriban asilimia arobaini ya dhahabu ya Afrika husafirishwa nje ya bara hilo kimagendo, ambapo kiwango kimeongezeka mara mbili katika muongo mmoja uliopita.


Tani kati ya mia tatu na mia nne za dhahabu, yenye thamani ya hadi dola bilioni thelathini na tano, zinazalishwa katika migodi midogo na kutokujulikana zinakoishia kila mwaka.


Swissaid inasisitiza kuwa dhahabu hiyo, ingawa ni chanzo cha mapato kwa wachimba madini na kodi kwa serikali za Afrika, pia inachangia katika kufadhili makundi ya waasi na kusababisha uvunjifu wa haki za binadamu na uchafuzi wa mazingira.


Ripoti hiyo, ambayo inaangazia kipindi cha kati ya mwaka 2012 na 2022 na imezingatia data kutoka nchi 54, inatoa mwanga katika changamoto za udhibiti na usimamizi wa rasilimali za Afrika, hususan katika sekta ya madini.

0 Comments:

Post a Comment